Home LOCAL MSAMA:  WAZAZI,  VIONGOZI WA DINI WASHAURINI VIJANA DHIDI YA VURUGU

MSAMA:  WAZAZI,  VIONGOZI WA DINI WASHAURINI VIJANA DHIDI YA VURUGU

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

MKURUGENZI wa Msama Promotion, Alex Msama, ameetoa wito kwa wazazi nchini kukaa karibu na watoto wao na kuwashauri kuepuka ushawishi wa kujiingiza kwenye vitendo vya vurugu na misukumo isiyo na tija.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Msama alisema wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha vijana wanalelewa katika misingi ya maadili na uzalendo, kwa kuwa wao ndio wamewazaa na kuwalea.

“Mimi kama mzazi niseme kuwa watoto ni wetu, tumewazaa na kuwalea. Tuna uwezo wa kukaa nao, kuzungumza nao na kuwaonya. Tusikubali waingie kwenye mkumbo wa kufanya vurugu,” amesema Msama.

Amesisitiza kuwa hakuna mtu mwenye mapenzi ya dhati kwa Tanzania zaidi ya Watanzania wenyewe, hivyo ni muhimu kuepuka kufuata mkumbo usio na manufaa kwa taifa.

“Amani tuliyonayo ni ya muhimu sana. Tumeachiwa na waasisi wetu, wazazi na mababu zetu. Tunapaswa kuilinda kwa nguvu zetu zote,” ameongeza.

Msama aliwahimiza pia viongozi wa dini kuendelea kuzungumza na waumini pamoja na vijana kuhusu umuhimu wa kulinda amani ya nchi, akisema historia ya vurugu haipaswi kurudiwa na kwamba taifa linapaswa kusonga mbele kwa misingi ya amani na upendo.

“Amani ni nguzo ya maendeleo. Tusirudi tulikotoka, tuijenge Tanzania yetu kwa amani na upendo,” amehitimisha.