Home LOCAL ZITTO: SITAKUBALI MWANANCHI APOKWE ARDHI BILA FIDIA KIGOMA

ZITTO: SITAKUBALI MWANANCHI APOKWE ARDHI BILA FIDIA KIGOMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Kutokana na kuwepo changamoto kwa baadhi ya wakazi wanaoishi katika jimbo la Kigoma mjini kutopata fidia pindi wanapoachia maeneo yao ili kupisha miradi ya kimaendeleo, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewaahidi wananchi kushughulika na changamoto hiyo atakapochaguliwa kuongoza jimbo hilo na chama chake kuongoza manispaa ya Kigoma ujiji.

Kauli hiyo imetolewa jana, Oktoba 20, 2025 na Zitto, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Majengo alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa chama hicho katika kata hiyo, Anzuruni Kibera.

Zitto amesema uamuzi wa serikali ya CCM kutowalipa fidia wananchi ni uvunjifu wa katiba ya nchi, ibara ya 24 inayopiga marufuku serikali au taasisi zake kutwaa eneo la mtu yeyote kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo bila kulipa fidia inayostahiki.

Ameyataja makundi ya wananchi wa jimbo hilo ambao hawajalipwa fidia ni pamoja na watu waliobomolewa makazi yao kupisha mradi wa KISEZ, kundi la pili ni waliovunjiwa nyumba zao kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma na kundi la tatu ni wakazi wa katubuka ambao nyumba zao zimezingirwa na maji.

“Kama mnapanua Airport hiyo ni shughuli ya kimaendeleo, kama mnajenga eneo la viwanda (KISEZ) hatukatai hayo ni maendeleo lakini ni lazima watu walipwe fidia inayostahiki kwa mujibu wa katiba na sheria, hili limekuwa ni tatizo haswa hapa Kigoma”, alisema Zitto

Zitto amewataka wananchi kujitokeza siku ya uchaguzi ili kuchagua viongozi watakaotokana na chama cha ACT Wazalendo, ili kuwapa nguvu ya pamoja kushughulika na changamoto hiyo na nyingine zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, mkoani Kigoma