Home LOCAL ZITTO AAHIDI NIDA, AIONYA CCM KIGOMA

ZITTO AAHIDI NIDA, AIONYA CCM KIGOMA

Mgombea ubunge wa jimbo la kigoma mjini kupitia ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameahidi kuwa atahakikisha kila mkazi wa jimbo hilo anakuwa na kitambulisho cha Nida, kwa sababu kila huduma nchini imeunganishwa na kitambulisho hicho.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Akiwa katika kata ya Rubuga jimboni hapo jana, Oktoba 21, 2025 amesema baadhi ya wakazi wa jimbo lake hawana vitambulisho hivyo kwa kuhisiwa kuwa raia wa nchi jirani za Burundi na Congo jambo linalowalazimu kukosa huduma mbalimbali za kijamii zilizounganishwa na vitambulisho hivyo.

“Mtu wa kigoma anaponyimwa kitambulisho cha Nida maana yake amenyimwa maisha hawezi kufanya chochote hawezi kuwa na namba ya simu, hawezi kuhudumia elimu ya mtoto wake, hawezi kuwa na bima ya afya, hawezi kufungua biashara yake wala kwenda hija,” alisema Zitto

Aliongeza kuwa endapo akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, atakwenda bungeni kutetea uraia wa wananchi wa jimbo hilo na mkoa wa kigoma, pamoja na haki ya wananchi kuwa na vitambulisho vya Nida.

Aidha alisema chama hicho kimejipanga kulinda kura zake na kudhibiti njama za udanganyifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

“Ninawaonya CCM tumeumwa na nyoka 2020, 2024, tutamuua huyo nyoka 2025 kabla hajatuuma tena, nataka tushindane kwa kura halali mshindi ampe mkono mshindwa tumalize”, aliongeza Zitto