Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa, na mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Watanzania wenzangu, Kazi na Utu?……
(Natumaini nyote mmeitikia, Tunasonga Mbele).
Mhe. Rais na Watanzania wenzangu, kwa majina ninaitwa Alex Msama Mwita.
Binafsi ni Mtanzania halisi, ninayetoka Kanda ya Ziwa, katika Mkoa wa Mara, makazi yangu ni Dar es Salaam, katika Manispaa ya Ilala, Jimbo la Uchaguzi la Ukonga, ambako nilitia nia ya kuomba nafasi ya Ubunge, ilivyo vyema ni kwamba Chama chetu kiliona wakati wangu bado, nami nilipokea kwa utiifu na unyenyekevu mkubwa maoni hayo.
Mimi Alex Msama, ni mwanachama na kada mwaminifu mwenye kiapo cha utiifu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kimaisha, mimi ni mfanyabiashara na muwekezaji wa kawaida, nikiwa Mkurugenzi wa Dira Media Group, Food Point, Msama Promotions na Msama Auction Mart.
Ninaandika waraka au barua hii ya wazi, kutoa maoni yangu binafsi, kama Ibara za 18, 21, 23 na 29 za Katiba ya Muungano wa Tanzania, zinavyoelekeza.
Mhe. Rais, nianze kwa kukupa pole nyingi kwa kazi kubwa unayoendelea nayo, kuzunguka mikoa mbalimbali hapa nchini, ukiwaelezea kwa kuwakumbusha Watanzania mambo mengi muhimu na makubwa yaliyofanywa na uongozi wako, kwa kipindi cha miaka minne na miezi kadhaa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Sanjari na kuwaomba kura za kishindo, mnamo Oktoba 29, mwaka katika Uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Rais, tangu Agosti 28, mwaka huu, zilipozinduliwa rasmi kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) pale viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe – Dar es Salaam, nimekuwa muumini mkubwa wa kufuatilia mikutano yako yote ya kunadi sera yakinifu za CCM kwa maendeleo thabiti ya Watanzania, hakika Mhe. Rais kazi unaifanya kwa wimo wa Moyo Mkuu.
Mhe. Rais, binafsi ninaposikiliza sera za chama na mawazo yako mwenyewe juu ya mabadiliko ya kimaendeleo kwa Watanzania na ninapokutazama usoni kupitia mboni za macho yako, naiona nuru inayoangaza dhamira halisi ya wewe kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mhe. Rais, kwa utafiti mdogo usio rasmi sana nilioufanya mimi Alex Msama, nimebaini pasina kificho kuwa matumaini makubwa ya Watanzania wameyaelekeza kwako na Serikali Imara itakayoundwa na CCM, baada ya Oktoba 29, 2025.
Aidha, Mhe. Rais, nichukue nafasi hii pia kukupongeza kwa kumaanisha kutoka katika viriba vya ndani ya moyo wangu, kwa namna ambavyo umekuwa na ngozi ngumu, moyo yabisi, fikra chanya na madhubuti kutokukatishwa tamaa na baadhi ya maneno ya hovyo kutoka kwa watu ambao wengine ni wewe umewasaidia kujipatia ‘ka umaarufu’ kidogo wanakotambia!
Zipo nyakati mimi Alex Msama huwa najaribu kuvaa viatu vyako nakuona ni binadamu wachache sana wenye uwezo wa kuvumilia na kustahimili upuuzi wa maneno ya kutunga unaoenezwa mitandaoni!
Mhe. Rais umetufundisha sisi Watanzania namna bora ya kukabiliana na uzushi wa watu wa hovyo, nayo ni kunyamaza na kuendelea kufanya maoinduzi kwa vitendo na kishindo cha mvumo wa radi.
Mhe. Rais unastahili pongeza za vifijo fungashi, kwa namna unavyopambana usiku na mchana kuhakikisha keki ya Taifa inawanufaisha Watanzania wote, lakini wakati huo huo watu ambao mimi nawaita vimelea, wanatumiwa na maadui wakubwa kukuvunja moyo, lakini bado upo imara na unasonga mbele, historia itakutetea kwa sentensi ndefu na kuliandika jina lako ‘Dkt. Samia Suluhu Hassan’, kwa WINO MPANA!
Naomba mwanao mimi Alex Msama, nikutie moyo Rais wetu, wewe ni Kiongozi mwenye maono makubwa mno.
Watanzania wengi wanajua thamani ya jasho lako katika kupambania na kupigania maendeleo yetu.
Dunia nzima imatambua uwezo wako wa kubadili yasiyowezekana kwa macho ya wengi, kuwa halisi.
Mimi Alex Msama nimebahatika kwa Neema ya Mungu kutembea maeneo mengi hapa nchini, Mhe. Rais, kazi ulizozifanya katika kuwahudumia Watanzania kwa huduma za kijamii, hazihitaji makelele na maelezo mengi, zinajitabainisha zenyewe, Watanzania ni mashahidi namba moja!
Mhe. Rais, una kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa mambo uliyoyafanya na kwa Ilani hii ya CCM iliyosheheni mambo makubwa, jina la Dkt. Samia litabaki vinywani mwa vizazi maelfu na maelfu vijavyo.
Mhe. Rais, kama Mtanzania unayo bahati ya kipekee kuliko yeyote.
Umeweka historia ya kuwa Makamu wa kwanza mwanamke, kwa kipindi cha miaka mitano na miezi mitatu.
Umeweka historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke kwa miaka minne na miezi kadhaa, mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa umeweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kupitishwa kwa kishindo na CCM kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na unakwenda kuwa Rais wa kwanza mwanamke kwa kupigiwa kura na Watanzania, wewe ni wa kipekee mno.
Mimi Alex Msama na wafanyakazi wenzangu wa Dira Media Group, Food Point, Msama Promotions na Msama Auction Mart, tunakuombea na Mungu, umalize salama siku za kampeni zilizobaki za kazi kubwa ya kukitafutia kura nyingi za kihistoria Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Watanzania tupo nyuma yako na tunaelewa nini unakifanya. Endelea kuwa imara huku ukimtumainia Mungu kwa kila hatua unayonyanyua unyayo kuipiga kwenda mbele.
Maadiko Matakatifu, kutoka katika Kitabu cha Isaya 41:10, Mungu anasema;
“Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu”.
Kitabu cha Yeremia 1:8, Mungu anasema;
“Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana”.
Mhe. Licha ya rekodi na historia uliyoweka kuwa mwanamke wa kwanza kushika nyazifa zote hizo, bado hauna majivuno, hauna maringo, mama hunyanyui mabega, Katika hilo Mungu akupe maisha marefu na fanaka tele.
Watanzania wenzangu, shime tuungane kwa umoja wetu kuilinda na kuipigania Amani ya nchi yetu, hii ndiyo Tunu pekee tunayojivunia katika uso wa Dunia hii.
Watu wachache kwa maslahi yao binafsi wasitupokonye Amani yetu, wakati wao wameshajitengenezea makazi huko ughaibuni.
Watanzania wenzangu, kuipoteza Amani ni jambo rahisi na jepesi sana lakini kuirejesha ni mzigo mzito wa maisha.
Tuendelee kupuuza kwa nguvu zetu zote maneno ya kutunga yanayozushwa na vimelea vyenye maslahi binafsi ya matumbo yao, tuilinde kwa wivu mkubwa Amani ya Taifa letu zuri tulilopewa na Mungu.
Nimalize waraka huu kwa kuwaomba, kuwasihi, kuwaasa na kuwakumbusha tena Watanzania wenzangu, Oktoba 29 mwaka huu, tujitokeze kwa wingi kukipigia kura kwa wingi Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atimize yale ambayo tunatamani yafanyike kwa ajili ya mstakabari wetu, kama Watanzania.
Kamwe tusikubali kucheleweshewa maendeleo tunayoyatamani na watu wachache waliojiandalia makazi yao na familia zao nje ya nchi.
Ndugu zangu Watanzania wenzangu, nitaendelea kuandika nyaraka (barua) hizi kwenu, kadiri nitakavyokuwa najaliwa ruzuku ya Oksijeni na Mwenyezi Mungu, ili kukumbushana mambo mengi muhimu yanayofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla, haya ni maoni yangu binafsi, sijaagizwa wala kuelekezwa na yeyote kuandika waraka huu.
Hii ni Salam yangu mimi Alex Msama Mwita, kwa mkono wangu mwenyewe.
Mungu awabariki sana;
Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.
Wenu katika Ujenzi wa Taifa,
Alex Msama Mwita;
Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) – Dira Media Group, Food Point, Msama Promotions & Msama Auction Mart.