KADA wa CCM, na Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama Mwita, ametoa wito kwa Watanzania kuzidi kupuuza minong’ono ya baadhi ya watu wanaotaja maandamano siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29 mwaka huu na badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura, kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo ya huduma za kijamii.
Akizungumza leo Oktoba 16, 2025, katika mahojiano maalum na baadhi ya waandishi wa habari alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya uzushi wa maandamano siku ya Oktoba 29, Msama aliwataka Watanzania kuziba pamba masikioni juu ya upotoshaji huo.
“Siku zote sisi Watanzania tumekuwa tukijivunia uungwana, utu, mshikamano, umoja, usikivu na Amani yetu, hayo mambo mengine yanabaki kuwa propaganda za watu wachache wasiopenda utulivu tulionao kama Watanzania.
“Niendelee kuwaomba Watanzania wenzangu, maana nimekuwa nikisema kila mara, kwamba katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, maneno mengi ya kuzusha yatakuwa mengi tuyapuuze,” alisema Msama na kuongeza;
“Binafsi ninayo Imani kubwa mno na Amiri Jeshi wetu Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninaviamini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo imara kwa ajili ya kulinda utulivu na Amani yetu.
“Watanzania wenzangu tujitokeze kwa wingi mnamo mwezi huu wa Oktoba tarehe 29, mwaka huu wa 2025, kupiga kura kuwachagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo tunayoyataka, nao si wengine bali wagombea wote wa CCM, kuanzi ngazi ya Rais wabunge na madiwani,” alisema Alex Msama.