
Wakazi wa Wete na maeneo jirani visiwani pemba, wamempongeza mgombea Urais Zanzibar, kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, (OMO),
kwa maono yake ya kuwekeza katika elimu na kumuenzi shujaa wa demokrasia visiwani humo, Marehemu Maalim Seif.
Wananchi hao wametoa pongezi hizo wakti wa mkutano wa hadhara wa mgombea huyo, uliofanyika wete Octoba 23, 2025, ambapo Bi Zainab Ali, alisema kiongozi huyo anazungumza kwa moyo kwani Maalim Seif alikuwa mtu mwenye kupenda na kithamini elimu.
“Kiongozi huyu anazungumza kwa moyo kwani Maalim Seif aliipendq elimu, na sasa tunaona mwendelezo wake kwa Othman. Hii ni neema kubwa kwa vijana wetu” alisema Bi.Zainab
Kwa upande wake, Mzee Khamis Abdalla, mmoja wa wazee wa mji huo, alisema kuwa amemwona Othman akisimamia misingi ya haki na elimu kama alivyofanya Maalim. Tukimpa nafasi, Zanzibar itarejea kwenye heshima yake ya kielimu na maendeleo.
Kikundi cha vijana wa Jadida kiliahidi kumpigia debe kwa nguvu zote, kikiimba kauli mbiu, “Elimu ni Ukombozi, Othman ni Tumaini!”
Kwa mujibu wa mpango wa awali wa chama hicho, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Maalim Seif Sharif Hamad unatarajiwa kuanza mara baada ya uchaguzi, kwa awamu ya kwanza ambayo itajumuisha majengo ya utawala, maktaba ya kisasa, na vitivo vya elimu, biashara, na teknolojia ya habari.
Chuo hicho kitapewa hadhi ya kimataifa, kikitoa nafasi kwa wanafunzi kutoka maeneo yote ya Afrika Mashariki, sambamba na programu za kubadilishana maarifa na vyuo vikuu vikubwa duniani.
Viongozi wa ACT Wazalendo wamesema kuwa ujenzi wa chuo hiki ni sehemu ya Dira ya Zanzibar Mpya, inayolenga kuimarisha elimu, ajira, na ubunifu miongoni mwa vijana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chuo hicho kitapokea zaidi ya wanafunzi 5,000 katika kipindi cha miaka mitano ya mwanzo, na kitatumia mifumo ya teknolojia ya kisasa katika ufundishaji ili kuandaa wataalamu watakaoipeleka Zanzibar katika uchumi wa kidigitali.
Wananchi wengi wamesema uamuzi wa Othman Masoud ni wa kipekee na unawapa matumaini makubwa.

Salum Abdalla, kijana kutoka Wingwi, alisema kuwa sera za Othman zinalenga kubadilisha maisha ya vijana kwa njia ya elimu. Alisema kuwa chuo hicho kitasaidia vijana wengi waliokuwa wanakosa nafasi za elimu ya juu Bara au nje ya nchi.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema kuwa wazo hilo linaonyesha dira ya kweli ya ACT Wazalendo katika kuwekeza kwenye maendeleo ya watu, si miundombinu pekee. Wamesema kuwa kujenga chuo kama hicho ni hatua ya kimkakati inayoweza kubadili taswira ya elimu Zanzibar.
Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Maalim Seif Sharif Hamad unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali ya ACT Wazalendo, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kiongozi huyo kuijenga Zanzibar yenye elimu, uadilifu na usawa kwa wote.
metolewa na Idara ya Habari na Uenezi
23 Oktoba 2025




