Home BUSINESS WAKANDARASI MRADI WA NHC SAMIA HOUSING SCHEME DODOMA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA...

WAKANDARASI MRADI WA NHC SAMIA HOUSING SCHEME DODOMA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UJENZI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

DODOMA

-Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt. Sophia Kongela amewataka wakandarasi na timu ya ujenzi ya mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) uliopo Medeli jijini Dodoma kuongeza kasi huku wakihakikisha ubora unabaki kuwa kipaumbele.

Ameyasema hayo wakati bodi hiyo ikikagua maendeleo ya mradi huo huku akipongeza hatua kubwa zilizofikiwa katika ujenzi huo jijini Dodoma.

Dkt.Kongela amesema kuwa,kasi iliyopo sasa ya ujenzi huo inapaswa kuongezeka ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

“Tunataka kuona kasi inaongezeka,mradi huu ni wa mfano na tunataka wateja wetu wafurahie makazi bora tuliyowaahidi,” amesema Dkt.Kongela.

Aidha,ameoneshwa kufurahishwa na ubunifu wa shirika katika kuhakikisha majengo yote ya mradi yana lifti na kila chumba kina master room, akisisitiza hatua hiyo inaonesha dhamira ya NHC katika kuboresha viwango vya makazi nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw.Hamad Abdallah amesema, shirika limejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya ubora wa hali ya juu na muda uliopangwa.

“Tupo kwenye kasi nzuri, na tunataka kuhakikisha Medali inakuwa alama ya makazi ya kisasa jijini Dodoma,”amesema Bw.Abdallah.

Mradi wa Samia Housing uliopo Medeli ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inayolenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora,ya kisasa na yenye gharama nafuu kwa Watanzania.

Mbali na hayo,Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imetembelea Estate ya Kikuyu jijini Dodoma na kufurahishwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na NHC Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuboresha mazingira ya makazi na kuongeza thamani ya nyumba za wapangaji.

Katika ziara hiyo, Bodi imeshuhudia kazi za ukarabati wa nyumba, uboreshaji wa miundombinu ya maji, umeme, mifereji ya maji ya mvua pamoja na mandhari ya jumla ya eneo hilo, hatua inayodhihirisha dhamira ya Shirika katika kutoa makazi bora, salama na yenye hadhi kwa wananchi.

Aidha, imepongeza Meneja wa Mkoa wa Dodoma na timu yake kwa usimamizi mzuri wa miradi na matumizi bora ya rasilimali, hatua inayosaidia kubadilisha taswira ya nyumba za NHC katika Jiji Kuu la Serikali.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Dodoma ameeleza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mpango mpana wa Shirika wa kuboresha Estates kongwe nchini ili ziendane na mahitaji ya sasa ya makazi ya kisasa.

NHC inaendelea kutekeleza mkakati wa kuhakikisha kila mkoa nchini unakuwa na nyumba zenye ubora unaoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.

Wakati huo huo,jumla ya nyumba 68 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu zimeendelea kuacha alama ya makazi bora katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma.

Kati ya nyumba hizo tayari nyumba 28 zimekwishauzwa huku zilizosalia zikiendelea kuchangamkiwa na wananchi.

Bodi ya NHC imeshuhudia moja kati ya nyumba hizo na kuridhishwa na utekelezaji wake na kuendelea kutoa pongezi kwa wahandisi wanaotekeleza mradi huo.

Katika mpango mkakati wake wa kuhakikisha nyumba 5000 zinajengwa sehemu mbalimbali nchini, sasa ni ujio waSamia Housing Scheme Njedengwa View Valley utakaohusisha maghorofa sita yenye nyumba 280 zikiwemo za chumba kimoja, viwili na vitatu.

Mradi huo ambao uko katika hatua za awali unatarajiwa kukata kiu ya wananchi wenye nia ya kumiliki nyumba katika jiji la Dodoma.

Huu ni wakati muafaka kwa wote wanaotaka makazi katika jiji la Dodoma kujipanga kikamilifu kuchangamkia fursa hii.