Home SPORTS TUTAPANDISHA THAMANI KAZI ZA SANAA NA MICHEZO- DKT. SAMIA

TUTAPANDISHA THAMANI KAZI ZA SANAA NA MICHEZO- DKT. SAMIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa katika Miaka mitano ijayo amedhamiria kupandisha thamani kazi za sanaa na michezo nchini kwa kulinda milki zao, kuhakikisha wanapata stahiki zao na kuwawezesha Vitendea kazi ikiwemo ujenzi wa studio kubwa na ya kisasa ya sanaa nchini.

Dkt. Samia pia ameahidi ujenzi wa kituo cha teknolojia bunifu katika jitihada zake za kukuza uchumi wa kidigitali, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo Vijana wa Kitanzania kuweza kuzifahamu fursa za uchumi wa Kidigitali pamoja na kuziendea fursa hizo ili kuweza kunufaika kiuchumi.

Dkt. Samia ameahidi hayo leo Jumanne Oktoba 28, 2025 siku Moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, wakati akifunga Kampeni za Chama Cha Mapinduzi kwenye Viwanja vya CCM Kirumba Mkoani Mwanza, akisisitiza ahadi yake pia ya kusimamia utungaji wa sera maalumu ya kutunza na kulea biashara bunifu za Vijana wa Tanzania.

Katika ahadi zake Nyingine, Dkt. Samia ameahidi kufanya utambuzi wa biashara ndogo nchini ikiwemo Biashara za Mamalishe na Baba lishe pamoja na biashara ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia Pikipiki na Bajaji ili kuweza kuzirasimisha, kuziingiza kwenye mipango ya nchi na kuwaendelea wafanyabiashara hao.

“Tutaenda pia kutafsiri Utu wa Mtanzania kwa vitendo kwa kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula, Maji safi na salama kwa kila Kaya, huduma stahiki za afya, elimu pamoja na ulinzi na usalama wa raia. Tutaendelea pia kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.” Amesisitiza Mgombea Urais huyo.

Aidha katika sekta ya madini, Dkt. Samia ameahidi kupima maeneo mapya ya uchimbaji wa madini ili kutimiza lengo la kutanua shughuli za kiuchumi kwa Vijana, jambo litakaloenda sambamba na ujenzi wa maabara za kisasa za Kanda pamoja na Kinu kikubwa cha kuchenjua madini nchini ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaongezewa thamani nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya Tanzania.