Home BUSINESS TUTAONDOA MAGUGU MAJI ZIWA BABATI NA KUNUNUA BOTI ZA UVUVI –...

TUTAONDOA MAGUGU MAJI ZIWA BABATI NA KUNUNUA BOTI ZA UVUVI – DKT.SAMIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutatua changamoto ya uwepo wa Magugu maji kwenye Ziwa Babati pamoja na maziwa mengine yote nchini yaliyoathiriwa na Mimea hiyo na hivyo kuathiri shughuli za uvuvi na shughuli nyingine za kijamii.

Dkt. Samia ameahidi hilo leo Jumamosi Oktoba 04, 2025 Mjini Babati kwenye Viwanja vya CCM Sabasaba ikiwa ni siku yake ya pili na ya mwisho ya kampeni zake Mkoani Manyara, akisema tayari serikali ya awamu ya sita imetoa fedha za kununua mtambo maalumu utakaotumika kwenye kuondoa mimea hiyo.

Kulingana na Dkt. Samia, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025/30 pamoja na mambo mengine imeelekeza kutekelezwa kwa mpango wa matumizi ya maeneo ya bahari na maji baridi kwa kushirikiana na wananchi ili maeneo hayo yaweze kuleta manufaa kwa wananchi wote.

Mgombea Urais huyo amerejea ahadi yake pia aliyoitoa jana Wilayani Hanang akisema ikiwa atapewa ridhaa na watanzania ya kuunda serikali, atanunua boti nne kwa Mkoa huo, tatu zikiwa ni za uvuvi na moja ya usalama ili kuendelea kutengeneza mazingira mazuri ya uvuvi kwa wananchi wa Mkoa huo.