Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, changamoto ya Maji na Umeme kwa Wilaya ya Meru na Tanzania kwa ujumla litakuwa historia, akiahidi huduma ya maji safi na salama pamoja na umeme wa uhakika kwa kila Mtanzania.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Meru Mkoani Arusha leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 kwenye Viwanja vya Kituo cha Mabasi Usa River, Dkt. Samia ameeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye miaka minne iliyopita katika sekta ya maji, akisema upatikanaji wa maji kwa Tanzania nzima sasa ni asilimia 87 na kabla ya Mwaka 2030 huduma ya maji itakuwa asilimia mia moja kote nchini Tanzania.
Amezungumzia pia changamoto ya Maji kwenye Wilaya ya Arumeru, akisema kwamba mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita itaenda kumaliza changamoto ya Maji kwenye wilaya hiyo, akihimiza umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji na miundombinu ya usambazaji maji.
Mgombea Urais huyo ameeleza pia kuhusu ajenda yake ya nishati safi nchini, akisema ajenda hiyo ni endelevu nchini ikidhamiria kuwanusuru Akinamama wa Tanzania dhidi ya madhara ya kiafya yanayotokana na nishati chafu za Kuni na Mkaa wakati wa kupika. Dkt. Samia kadhalika ameahidi kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya kilimo nchini ili kufikia dhima ya sekta hiyo kukua kwa asilimia kumi kufikia mwaka 2030, wakitia juhudi zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ili kukuza uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima wa Tanzania.