
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kukamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Buyango Wilayani Missenyi Mkoani Kagera ili kuendelea kutoa fursa ya Vijana kupata ujuzi wa kuweza kuajiriwa na kujiajiri katika jitihada za serikali za kuondokana na tatizo la ajira kwa Vijana wa Kitanzania.
Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo Kyaka, Misenyi Mkoani Kagera leo Jumatano Oktoba 15, 2025 wakati akiomba kura kwa wananchi wa Wilaya hiyo, kwenye muendelezo wa Kampeni zake kuelekea Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akiahidi pia kuendelea na sera yake ya ada bila malipo kwa wanafunzi wote wa shule za msingi mpaka wanafunzi wa Kidato cha sita.
Kwa Wilaya ya Missenyi, Dkt. Samia amesema serikali ya awamu ya sita imetoa Bilioni saba na Milioni mia mbili kugharamia sera hiyo ya elimu bila ada, akisema fedha hizo isingekuwa Sera yake ya Elimu bila ada, gharama zote hizo zingegharamiwa na Wazazi na walezi wa wanafunzi hao bila kujali hali ya uchumi wa familia za wanafunzi hao.
Amezungumzia pia mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya afya Wilayani Misenyi, akisema Shilingi Bilioni tatu na Milioni mia nane zimetolewa kwa miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, zikiwezesha ujenzi wa Majengo 13 kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misenyi, ununuzi wa vifaatiba na madawa, Ujenzi wa Vituo vitatu vya afya na Zahanati saba pamoja na ununuzi wa magari matatu ya kubebea wagonjwa wa dharura.
Ameahidi pia kujenga barabara ya urefu wa Kilomita mbili kwa kiwango cha lami kutoka Kona ya Bulembo hadi kwenye Hospitali hiyo ya Wilaya ili kurahisisha shughuli za usafiri kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali hiyo.
Kwa miaka minne ya serikali ya Dkt. Samia, Wilaya hiyo pia imenufaika na ujenzi wa shule mpya saba za msingi, Mabwemi 12 na madarasa mapya 112 huku pia zikijengwa shule mpya 3 za Sekondari. Dkt. Samia ameahidi kuwa ikiwa atachaguliwa kwenye Uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Serikali yake pia itaendelea kusogeza na kuboresha huduma muhimu za kijamii Wilayani humo ikiwemo huduma za maji safi na salama, huduma za maji, umeme na afya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji.





