

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo, serikali atakayoiunda ikiwa atapewa ridhaa itajenga barabara za juu (Flyover) kwenye makutano ya barabara za Mwenge, Morocco, Magomeni na barabara ya Ali Hassan Mwinyi na United Nation Jijini Dar Es Salaam.
Ahadi ya Dkt. Samia ameitoa leo Jumanne Oktoba 21, 2025 wakati wa mkutano wake wa Kampeni kwenye Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar Es Salaam, akisisitiza kuwa lengo ni kupunguza msongamano, kuongeza ufanisi wa barabara na kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii Mkoani humo.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia pia mbele ya maelfu ya wananchi wa Majimbo ya Kinondoni, Kibamba, Ubungo na Kawe, ameahidi pia kushughulikia maeneo yenye kukabiliwa na changamoto ya mafuriko Jijini Dar Es Salaam ikiwemo Mto Mbezi, Mto China na Mto Gide akisema Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) awamu ya pili utaondoa changamoto hizo.
Amesema katika utekelezaji wake watajenga na kukamilisha pia mifereji ya Maji ya mvua katika maeneo ya Tandale, Magomeni na Makumbusho ili kuondoa adha ya mafuriko katika maeneo hayo ya Kinondoni Jijini humo.
Kwa upande wa barabara, Dkt. Samia amesema ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, atakamilisha ujenzi wa barabara ya Kimara- Mavurunza- Bunyokwa- Kinyerezi, yenye urefu wa Kilomita saba, barabara muhimu kwa maendeleo ya Majimbo matatu ya Segerea, Kibamba na Ubungo.
Aidha pia ameahidi kutekeleza miradi mipya katika Wilaya hiyo ikiwemo upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki sehemu ya Kilomita tisa kutoka Morocco hadi Kawe na barabara ya Garden (Garden road) pamoja na barabara ya Tegeta- Bagamoyo yenye jumla ya urefu wa Kilomita 57 na kukamilisha barabara ya Kibamba- Mloganzila, sehemu ya Mloganzila mpaka Mloganzila Citizen yenye urefu wa Kilomita nane.





