
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa serikali imetangaza Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa wenye sifa za kupiga kura, kushiriko kuchagua Viongozi wanaowataka bila vikwazo, akibainisha kwamba Vyombo vya ulinzi na usalama vimetoa hakikisho pia la mazingira salama na utulivu wakati wote wa uchaguzi na hata baada ya upigaji kura.
Dkt. Samia kufuatia hali hiyo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mwanza kwenye Viwanja vya CCM Kirumba Jijini Mwanza wakati wa ufungaji wa Kampeni zake za uchaguzi Mkuu, ametoa rai pia kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kuhamasishana kwenda kupiga kura.
“Ndugu zangu wananchi kwa pamoja tumefanya kazi ya kunadi Ilani ya CCM nawashukuru kwa kufanya kampeni za kistaarabu na zilizotawaliwa na hoja na sio kuzodoana, mmeonesha njia kwa vyama vingine kuendana na ukomavu wetu wa kidemokrasia. Vilevile navipongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendesha kampeni za kiungwana na kushindana kwa hoja. Tumeshindana kwenye kujieleza namna tutakavyotekeleza ahadi zetu kwa wananchi wakituchagua na sasa ni wakati wa kushindana kwenye maboksi ya kura.”
Niombea Vyama vya siasa kuwa na utulivu na kuachia wananchi wafanye maamuzi yao. Ndugu zangu kupiga kura ni haki yako ili kuweza kuweka madarakani Viongozi unaoona watakutendea mema mkiwachagua, niwatake watanzania twende kwa wingi kupiga kura ili tuimarishe demokrasia. Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha ndugu zangu wana CCM na wapenzi wa Chama chetu kwamba shabaha yetu ni kushinda uchaguzi huu tena ushindi wa heshima.
“Hakuna upinzani dhaifu wala upinzani mwepesi, twendeni kwa nguvu zote, tusiseme upinzani ulipo dhaifu au mwepesi, hapana, twendeni kwa nguvu zote tukachague Wagombea wa Chama Cha Mapinduzi, twendeni tukachague Kazi na Utu, twendeni tukachague CCM.” Amesisitiza Dkt. Samia.





