Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza dhamira na mpango wake wa kuendeleza sekta ya maziwa nchini, kwa kuwawezesha wafugaji wa Ng’ombe wa maziwa sambamba na kujenga Viwanda vya kuongeza thamani zao hilo ili kukuza tija kwa wafugaji kupitia masoko ya maziwa.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Jumapili Oktoba 12, 2025 kwenye Viwanja vys shule ya Msingi Ushirombo, Wilayani Bukombe Mkoani Geita kwenye siku yake ya kwanza ya Kampeni Mkoani humo, akisisitiza pia kuendelea na utoaji wa ruzuku za chanjo kwa mifugo, kujenga majosho, kujenga na kukarabati minada ya mifugo pamoja na ujenzi wa machinjio za kisasa ili kukuza tija ya sekta hiyo.
“Bukombe hii ina wafugaji wa kawaida wa ng’ombe wa nyama lakini ng’ombe wa maziwa. Tunachojipanga serikali yenu watu wa Bukombe mbali ya kuongeza nguvu kwenye sekta ha mifugo kwa ujumla, tumeamua sasa tuingie kwenye ng’ombe wa maziwa, tuinyanyue sekta ya biashara ya maziwa ambapo Bukombe ni wazalishaji wa maziwa wazuri sana. Tunaenda kuinyanyua sekta ya maziwa lakini pia kuweka Viwanda vitakavyochakata maziwa ili maziwa yawe bidhaa na wafugaji wale waweze kuuza, fedha iingie mfukoni na hiyo ndiyo kazi na utu.” Amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia pia amezungumza kuhusu michezo Wilayani Bukombe kama sehemu ya burudani, akisema serikali yake inajenga uwanja wa Kisasa Wilayani humo kwa fedha za serikali na wadau wengine wa michezo ikiwemo kampuni ya Azam Limited ambao wametoa taa kwaajili ya kufunga ndani ya uwanja huo wa kisasa.