Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza dhamira yake ya kukuza hadhi ya Jiji la Mwanza kwa kuendelea kuhakikisha huduma zote muhimu za kijamii zinakuwa za uhakika kwa kila mwananchi ikiwa atachaguliwa na kupewa ridhaa ya kuunda serikali kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Dkt. Samia ameyaeleza hayo leo Jumanne Oktoba 07, 2025 kwenye Viwanja vya Kituo cha Mabasi Buhongwa, Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza, aliposimama na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo kwenye siku yake ya kwanza Mkoani humo, akibainisha kuwa atasimamia miradi yote pia iliyoanza iweze kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kusudiwa.
Ametaja Miundombinu atakayoenda kusimamia ujenzi wake kuwa ni pamoja na umaliziaji wa reli ya Kisasa ya SGR kipande cha Mwanza pamoja na ujenzi wa masoko ya Mchafu kuoga, Soko la samaki Mkuyuni, soko la mbao Nyegezi, soko la mazao Igoma pamoja na masoko ya Mabatini, Tambukareli, Buhongwa, Bukarika pamoja na Butimba.
“Masoko haya yote tutayajengwa kwa kushirikiana na Halmashauri na ahadi yetu ni kuendelea kuiboresha Mwanza na kuitengeneza liwe Jiji kwelikweli” amesisitiza Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza pia mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ya serikali yake ya awamu ya sita ikiwemo ujenzi wa Kituo kikuu cha mabasi Nyegezi, Soko kuu la Mjini Kati, maboresho katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Vituo vipya 4 vya afya pamoja na ujenzi wa shule mpya 6 za Sekondari, nane za Msingi na Mabweni mawili kwa shule ya msingi ya watoto wenye mahitaji maalumu Buhongwa.
Aidha Katika sekta ya Maji, Serikali yake pia imefanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji uliogharimu zaidi ya Bilionu sabini na moja na Milioni mia saba, mradi unaohudumia wananchi 450,000 wa Kata za Buhongwa, Nyegezi na Igoma.
Serikali ya Dkt. Samia pia imewezesha kuondoa tatizo la kukatika kwa Maji mara kwa mara, pamoja na ujenzi wa matenki makubwa ya maji yenye kuhifadhi lita Milioni tano na kumi katika maeneo ya miinuko, sehemu ambazo zilikuwa zikikosa maji kutokana na presha ya maji kuwa ndogo kuweza kupandisha maji kwenye maeneo hayo ya miinuko.