


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) Bw. Gilead Teri, akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2025, jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Bakari Machumu akizungumza katika kikao kazi na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kilichofanyika leo, Oktoba 23, 2025, jijini Dar es Salaam.
Na; Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) Bw. Bw. Gilead Teri, amesema Mamlaka hiyo imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inasajili miradi 1,500 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 15, ifikapo mwaka 2026
Teri, ameyasema hayo katika kikao kazi kati ya Taasisi hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika Octoba 23, 2025 Jijini Dar es Salaam, ambapo amebainisha kuwa mikakati hiyo inakwenda sambamba na kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Uwekezaji una manufaa mengi ikiwemo kuongeza mitaji, ajira, mapato ya kodi, pamoja na kuleta teknolojia mpya na za kisasa katika uchumi wa nchi.
“Hapa tunalenga kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hatua itakayowanufaisha moja kwa moja wawekezaji, makampuni na Taifa kwa ujumla” Amesema.
Ameongeza kuwa TISEZA, inaendelea kuandaa uzinduzi wa huduma katika eneo maalum la kiuchumi la Ubungo, ambapo watatoa huduma bure kwa Watanzania wanaotaka kuuza bidhaa zao nje ya nchi, na kujifunza namna ya kuagiza mitambo kwa ajili ya kuanzisha viwanda.
Pia, amewasihi wahariri wa vyombo vya habari nchini, kuendelea kuhabarisha umma kuhusu mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea, chini ya uongozi wa Mheshiiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Bakari Machumu, ameipongeza TISEZA kwa hatua ya kuwaelimisha wahariri kuhusu utekelezaji wa majukumu yake na sheria mpya ya uwekezaji.
“Kikao hiki kimetupa uelewa mpana kuhusu TISEZA na sheria mpya ya uwekezaji. Hii itatuwezesha kuandika kwa usahihi, kuuliza maswali sahihi, na kuchochea maboresho katika sekta ya uwekezaji nchini” amesema.








