Home BUSINESS SERIKALI YAINGIZA MABASI 60 NJIA YA KIVUKONI-KIMARA-MAJALIWA

SERIKALI YAINGIZA MABASI 60 NJIA YA KIVUKONI-KIMARA-MAJALIWA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

_Asema sasa njia hiyo itakuwa na mabasi 90_

_Asema lengo ni kuhakikisha kero ya usafiri katika njia hiyo inakwisha_

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye Barabara ya mabasi yaendayo haraka njia ya Kimara hadi Kivukoni iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu wa magari uliokuwepo.

Amesema kuwa idadi hiyo itafanya njia hiyo kuwa na mabasi 90 ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuondoa kero ya usafiri iliyokuwepo katika kipindi cha hivi karibuni.

Amesema hayo leo Alhamisi ( Oktoba 02, 2025) alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri kwa mabasi yaendayo haraka kwa njia ya Kivukoni hadi Kimara jijini Dar es Salaam.

“Serikali yenu baada ya kuruhusu makampuni binafsi tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo, malengo yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza UDART na DART kuhakikisha wanasimamia matumizi ya kadi za kielektroniki katika utozaji wa nauli badala ya kutumia fedha taslimu (Cash) ili kudhibiti upotevu wa mapato katika usafiri huo.

“Na tumeagiza kadi hizi zisiwe za mabasi haya pekeyake, tunataka zitumike kwenye viwanja vya mipira, usafiri wa Azam marine, SGR, vituo vya mabasi, Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry Silaa, tunataka hili likamilike kwa haraka”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Dart kuhakikisha wanasimamia kikamilifu usafiri huo ili kupunguza kero ya usafiri wa mabasi hayo katika jiji la Dar es Salaam.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuiamini Serikali kwamba itahakikisha kero ya usafiri katika njia hizo itapunguzwa kwa kiasi kikubwa ili kuondoa tatizo la usafiri katika jiji la Dar es Salaam. “Haya yaliyojitokeza tuamini sasa yamekwisha”

Akizungumzia kuhusu maboresho hayo, Mmoja ya wasafiri amesema kuwa usafiri katika siku hiyo umekuwa wa kuridhisha na wanasafiri kwa wakati “Kwasiku ya leo usafiri umekuwa mzuri na magari yameingia kwa wakati”