Home LOCAL SERIKALI YA ACT KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

SERIKALI YA ACT KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Serikali ya ACT Wazalendo imeahidi kushughulikia kwa kina masuala ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto mara itakapoingia madarakani.

Kauli hiyo imetolewa na Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Mheshimiwa Othman Masoud, alipokutana na walimu wa madrasa pamoja na watu mashuhuri kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Micheweni, Pemba.

Katika mazungumzo hayo, baadhi ya viongozi wa dini walieleza kwa masikitiko makubwa juu ya kuongezeka kwa vitendo vya ukatili, hususan dhidi ya watoto wadogo, jambo ambalo limekuwa likiiaibisha jamii na kupunguza heshima ya maadili.

Othman Masoud alisema Zanzibar haiwezi kuwa sehemu ya kuvumilia watenda maovu na kusisitiza kuwa sheria lazima zifuate mkondo wake bila upendeleo.

Alibainisha kuwa Serikali itakayoongozwa naye itahakikisha inachukua hatua madhubuti za kupambana na vitendo hivyo na kulinda haki za wanawake na watoto.

Aidha, aliongeza kuwa kwa zama na zama Zanzibar imejulikana kama nchi ya visiwa yenye kufuata misingi ya dini, lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na kuongezeka kwa mambo yasiyo na msingi katika jamii.

Alisema ni wajibu wa viongozi wa dini, wazazi na walimu kushirikiana katika kuirejesha jamii kwenye maadili mema na misingi ya heshima.

Sambamba na hilo, Othman alisema udhalilishaji umekuwa ukijitokeza katika maeneo tofauti ambayo mara nyingi wanakutana nayo watoto wa kike.

Akitolea mfano, alisema kukosa ajira kwa vijana wa kike ni aina nyingine ya udhalilishaji wa kimfumo unaosahaulika na kutopewa uzito unaostahili. Alifafanua kuwa changamoto hiyo huwafanya vijana wengi wa kike kuwa katika mazingira hatarishi, jambo linaloweza kuchangia vitendo vya unyanyasaji na ukosefu wa heshima katika jamii.

Aliahidi kuwa Serikali yake itashughulikia kwa ukamilifu mkubwa suala la ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wote, hasa kwa wanawake, kwa kuhakikisha kila kijana ana nafasi ya kujiajiri au kupata kazi yenye staha.

Othman alisema Serikali ya ACT itatengeneza mazingira rafiki ya ujasiriamali, mafunzo ya ufundi, na mikopo midogo itakayowezesha vijana kujiendeleza kimaisha, ili kupunguza utegemezi unaochochea udhalilishaji wa kijinsia.

Akiendelea kuzungumza, Othman aliahidi pia kuanzisha mabaraza maalum ya maadili na usalama wa kijamii katika kila wilaya, ambayo yatashughulikia kwa haraka kesi za ukatili wa kijinsia na kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga.

Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa jamii nzima, hivyo Serikali ya ACT itahakikisha elimu ya kinga na ulinzi wa watoto inatolewa mashuleni na kwenye taasisi za dini ili kulinda kizazi kijacho.

Mapema Sheikh Ali Juma Hamad wa Wingwi alisema kuwa imekuwa aibu sasaivi suala udhalilishaji wa wanawake na watoto katika jamii ya Zanzibar.

“Unasikia mzee wa miaka 70 anamuingilia Mtoto wa miaka mitano jamanii ndio tulipofikia hapaa, Mgombea tunapoteza vitendae kazi vya mbelee” alieleza Sheikh Ali

*Imetolewa na Idara ya Habari na Uenezi.ACT Wazalendo*
*15 Oktoba 2028*