Home BUSINESS OTHMAN KUFANYA MABADILIKO MAKUBWA VISIWA VIDOGO VIDOGO UNGUJA, PEMBA

OTHMAN KUFANYA MABADILIKO MAKUBWA VISIWA VIDOGO VIDOGO UNGUJA, PEMBA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vya Zanzibar, akisisitiza kwamba Serikali yake itahakikisha kila Mzanzibari anahisi kuwa sehemu ya nchi bila kujali umbali alipo.

Othman aliyasema hayo mara baada ya kuwasili Kisiwa cha Fundo, kilichopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, eneo lililopo umbali wa takribani kilomita 10 kutoka bandari ya Wete, safari inayochukua takribani dakika 30 kwa mashua ndogo kupitia Bahari ya Hindi.

Kisiwa hicho, chenye wakazi wapatao watu 1,200, kimekuwa miongoni mwa maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Othman alisema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuvithamini visiwa vidogo licha ya mchango mkubwa wanaoutoa kupitia sekta ya uvuvi. Alisisitiza kuwa katika Serikali atakayoiongoza yeye, atahakikisha wananchi wote wanaoishi kwenye visiwa wanapata huduma stahiki kama ilivyo kwa wananchi wanaoishi mijini.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali yake itaweka mifumo bora ya kuimarisha sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia wavuvi boti za kisasa zitakazowawezesha kufika katika kina kirefu cha bahari kwa usalama zaidi, sambamba na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi na kusindika samaki.

Aliahidi pia kuboresha huduma za afya, hasa huduma za uzazi kwa wajawazito, ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Fundo na visiwa jirani. Alisema kuwa ni aibu kuona mama wajawazito wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za haraka, hivyo Serikali yake itahakikisha zahanati za kisasa zinajengwa katika kila kisiwa, zikiwa na madaktari na vifaa vya kisasa.

Katika sekta ya elimu, Othman alisema ataunda mifumo ya elimu inayozingatia mazingira ya bahari na uvuvi ili kuwapa vijana wa visiwani ujuzi wa kujiajiri na kuchochea uchumi wa maeneo yao.

Alisema vijana wa visiwani wana uwezo mkubwa wa kubadili maisha yao, wanachohitaji ni mazingira bora ya kujifunza na kufanya kazi.

Wakazi wa Kisiwa cha Fundo walimshukuru Mgombea huyo kwa kufika katika eneo lao ambalo mara chache hutembelewa na viongozi wakuu, wakieleza kuwa ujio wake umeonesha dhamira ya kweli ya ACT Wazalendo katika kujenga Zanzibar yenye usawa.

Mzee Khamis Salim, mkazi wa Fundo, alisema ujio wa Othman Masoud ni ishara ya matumaini kwao na kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakisahaulika. Alisema wameguswa na ahadi zake na wako tayari kumpa kura zao zote ifikapo siku ya uchaguzi.

“Tumepata matumaini makubwa. Tumemsikiliza kwa makini, na tumeona anajua matatizo ya watu wa visiwani. Sisi wazee wa Fundo tumeamua, kura zetu zote ni za Othman Masoud,” alisema Mzee Khamis kwa niaba ya wazee wenzake.

Naye Bi. Mwanakhamis Abdalla, alisema wananchi wa Fundo wanataka kiongozi atakayewakumbuka baada ya uchaguzi, siyo kuja na ahadi zisizotekelezeka. Alisema wameamini kuwa Othman ni kiongozi mwenye nia njema kwa wanyonge.

Wazee wa kisiwa hicho walimuahidi Mgombea huyo kumpa kura zote za kisiwa hicho wakiamini kuwa ni mkombozi wao atakabadilisha maisha ya kisiwa hicho.

Kwa kauli na ahadi zake, Othman Masoud ameendelea kujijengea taswira ya kiongozi anayegusa maisha ya kila Mzanzibari, hata wale wanaoishi mbali zaidi na miji mikuu, akithibitisha kuwa maendeleo ya kweli hayana mipaka ya bahari.

Mwisho

Imetolewa na Idara ya Habari na Uenezi*
4 Oktoba 2025