Home LOCAL OMO ATIKISA NUNGWI AKIOMBA KURA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR

OMO ATIKISA NUNGWI AKIOMBA KURA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman (OMO) ameendelea kuwasha moto wa kampeni visiwani Zanzibar, akihutubia maelfu ya wananchi na wanachama katika mkutano uliofurika Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika mkutano huo Othman amesisitiza kuwa wakati wa mabadiliko umefika na kwamba safari ya ushindi sasa imepata kasi ya upepo wa bahari ya mabadiliko.

Othman amesema anaamini kwa dhati kuwa ushindi wa ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 si jambo la ndoto tena bali ni uhalisia unaoonekana kwa macho, akisisitiza kuwa chama chake kina mtandao mpana wa wanachama, vijana, na wazalendo wanaotaka kuona Zanzibar mpya yenye uwajibikaji na heshima kwa wananchi wake.

Amesema chama chake kina idadi kubwa ya wanachama kuliko CCM, hivyo ushindi kwao ni jambo lililo wazi, kwani wananchi wameshachoka na ahadi zisizo na utekelezaji.

Ameongeza kuwa wanakwenda kwenye uchaguzi huo wakiwa washindi tayari, na jukumu lao kubwa ni kulinda ushindi wa wananchi.

Akiwa na hamasa kubwa, Othman aliahidi kuwa serikali itakayoongozwa na ACT Wazalendo itachukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika na ufisadi na uporaji wa mali za umma, akisisitiza kuwa zama za kulindana zimekwisha.

Alieleza kuwa huu ndio mwisho wa utawala wa CCM, kwa sababu wananchi wamewachoka.

Alifafanua pia kuwa ndani ya CCM kuna viongozi wakubwa wasioridhishwa na uongozi wa Rais Mwinyi, jambo linaloonyesha kuwa chama hicho kimepoteza umoja na mwelekeo.

Othman alisema kuwa CCM hawana tena mtandao wa watu, bali wamebaki na ujanja na ghilba, lakini safari hii hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wananchi wameamka na hawatapokonywa haki yao tena.

Aliongeza kuwa kwa sasa CCM kinachopaswa kufanya ni kujiandaa kuwa washiriki wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama mshindi wa pili, kwani huo ndio ukweli wa kisiasa ulivyo.

Alisema maandalizi hayo kisaikolojia yatawasaidia kuondoka madarakani kwa heshima bila fedheha.

Awali, Mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, aliwahimiza wananchi wa Zanzibar kutafakari hatma ya nchi yao kwa kina. Alisema huu si muda wa kuendeleza misimamo ya kichama, bali ni wakati wa kuenzi uzalendo na kuokoa taifa.

Aliongeza kuwa Zanzibar imefikia hatua ngumu inayohitaji uamuzi wa busara, na kwamba wakufanya hivyo ni wananchi wenyewe, kwani wao ndio wenye mamlaka halisi ya kuamua mustakabali wa nchi yao.