
Monday, October 27, 2025
Na: Mwandishi Wetu, Kahama na Nzega
Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwanasiasa mkongwe, Khamisi Mgeja, amewatahadharisha Watanzania kuepuka kufanya makosa katika uchaguzi ujao kwa kumchagua rais asiye na uzoefu, akisisitiza kuwa nafasi ya urais haijaribiwi.
Mgeja amesema yatakuwa makosa makubwa kumpa nafasi ya uongozi mtu ambaye hajawahi kushika majukumu yoyote ya kiutawala, hasa wakati ambapo Dk. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais wa CCM, “yupo na anatosha” kuendelea kuiongoza Tanzania.
Akizungumza leo, Oktoba 27, katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika wilaya za Nzega mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga, Mgeja amesema Dk. Samia ni kiongozi mwenye rekodi ya utekelezaji na anastahili kupewa ridhaa ya kuendelea na kazi aliyoianza ya kuijenga nchi.
“Urais si nafasi ya majaribio. Tuna kiongozi ambaye ameonyesha uwezo, uthubutu na matokeo makubwa ya maendeleo katika sekta zote,Mama yetu Dk. Samia anatosha kabisa,Sasa ni zamu yetu kumlipa kwa kura za heshima na kishindo tarehe 29,” amesema Mgeja.
Mgeja pia ametumia jukwaa hilo kuwaomba wananchi wa Nzega na Kahama kuwapigia kura wagombea wa CCM akiwemo Hussein Bashe, Mgombea Ubunge wa Nzega, na Benjamin Ngayiwa, Mgombea Ubunge wa Kahama Mjini, pamoja na madiwani wa chama hicho.
Akiwa katika vijiji vya Nyanhembe na Ufala wilayani Kahama, amesisitiza kuwa Bashe na Ngayiwa ni vijana wachapa kazi wenye dira ya maendeleo na wanastahili kupewa nafasi ya kuwatumikia wananchi.
“Benjamini ni kijana mwenye ari kubwa na dhamira njema kwa wananchi wa Kahama Mjini,na Bashe, kupitia Wizara ya Kilimo, ameonyesha uongozi wenye matokeo makubwa,ni wakati wa kuwapa tena dhamana ili waendeleze kazi nzuri waliyoanza,” amesema.
Katika maelezo yake, Mgeja amewakumbusha Watanzania maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema kuwa “Kiongozi bora wa Tanzania hawezi kutoka nje ya CCM, bali kutoka ndani ya CCM.”
Amesema kauli hiyo inathibitishwa na utendaji wa Dk. Samia ambaye ameonyesha kuwa ni kiongozi wa watu, mwenye maono, utu, na dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
“Dk. Samia ni mama mwenye imani, utu na moyo wa maendeleo,amefanya kazi kubwa na ninaamini yajayo ni mazuri zaidi,huu si wakati wa majaribio,” amesisitiza Mgeja.
Aidha, Mgeja amesema umoja na mshikamano wa taifa uko imara chini ya uongozi wa Dk. Samia, akibainisha kuwa Tanzania ipo salama na inaendelea kuimarika kisiasa na kiuchumi.
Amewaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi na kutokubali kurubuniwa na watu wanaochochea chuki au vurugu wakiwa nje ya nchi kwa maslahi binafsi.
“Wapo wanaotumiwa na mabeberu kujaribu kuleta vurugu nchini. Watanzania tusikubali. Tuendelee kuamini chama chetu, serikali yetu na kiongozi wetu Dk. Samia,” amesema.
Mwisho





