Katika siku za hivi karibuni, Zanzibar imeshuhudia hamasa kubwa ya wananchi katika mikutano ya hadhara inayoongozwa na Othman Masoud. Kutoka mitaa ya Mjini Unguja hadi vijiji vya mbali kisiwani Pemba, maelfu ya wananchi wamejitokeza kwa wingi, wakijazana viwanjani kusikiliza ujumbe wake.
Hali hii imekuwa ikitafsiriwa kama ishara ya kiu ya mabadiliko na matarajio mapya kwa mustakabali wa Zanzibar.
Wananchi wa Unguja mjini wameonekana kuvutiwa na kauli zake zinazogusa maisha ya kila siku, hususan suala la ajira na gharama za maisha. Vijijini Pemba, mapokezi ya wakulima na wavuvi yamekuwa ya dhati, wakionesha imani kwa kiongozi anayewasikiliza na kuelewa changamoto zao.
Mikutano yake haijabaki kuwa maneno matupu, bali imekuwa chombo cha kujenga matumaini mapya kwamba mabadiliko yanawezekana.
Kwa mfano, Othman ameonyesha jinsi uwekezaji wa kilimo na uvuvi unaweza kubadilisha maisha ya vijijini.
Kwa kufungua masoko ya karafuu na bidhaa nyingine za kilimo, wakulima wataweza kuuza mazao yao kwa bei halisi, badala ya kulazimishwa kuuza kwa madalali wanaowapotezea faida.
Vilevile, kupitia uwekezaji wa uvuvi wa kisasa, wavuvi wataweza kuongeza uzalishaji na kupata faida zaidi, bila kutegemea madalali au masoko ya nje yenye vikwazo.
Kwa wengi, Othman Masoud sasa anaonekana kama kinara wa mabadiliko Zanzibar. Wananchi wanamwona kama kiongozi mwenye uthubutu wa kuondoa mfumo unaowanufaisha wachache huku wengi wakisalia kwenye umasikini.
Uwazi wake, ukaribu wake na wananchi, na ahadi zake zenye kutazama uhalisia wa maisha ya watu, vimezidi kumjenga kama kiongozi anayehitajika kwa zama hizi.
Othman ameahidi kubadilisha mfumo wa elimu ili vijana wa Zanzibar wajifunze fani zinazolingana na mazingira yao, kama kilimo, uvuvi, utalii na teknolojia.
Hii itawapa uwezo wa kujiajiri wenyewe na kuendesha miradi midogo, badala ya kutegemea ajira zisizo na uhakika.
Kiwango cha chini cha mshahara kuwa milioni moja ni moja ya ahadi kubwa zilizowavutia wananchi.
Hii imepokelewa kwa hisia kubwa na wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi ambao kwa muda mrefu wamelalamikia mishahara midogo isiyoendana na gharama za maisha.
Aidha, Othman ameahidi kurejesha heshima ya walimu na watumishi wa umma, ili mchango wao kwa taifa utakumbukwa na kuthaminiwa.
Katika sekta ya afya, Othman ameeleza wazi kuwa mfumo wa bima ya afya Zanzibar umejaa ufisadi na unawakamua wafanyakazi, badala ya kuwanufaisha.
Amepanga kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kila mzanzibari anapata huduma bora bila kutozwa gharama zisizo za lazima.
Aidha, Othman ameahidi kupambana na uwekezaji holela unaoharibu ardhi za wananchi na kuhakikisha miradi yote inazingatia maslahi ya wazalishaji wa ndani.
Kwa mfano, uwekezaji wa viwanda vidogo vya kutengeneza bidhaa za kienyeji unaweza kuongeza ajira, kupunguza umasikini, na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi.
Othman ameahidi kuifungua Zanzibar kimataifa, akitumia rasilimali za ndani kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kidiplomasia na kijamii.
Lengo ni kuhakikisha Zanzibar inapata nafasi muhimu katika ramani ya biashara, utalii na elimu.
Mfano ni katika sekta ya mafuta na gesi. Othman ameahidi kuwa rasilimali hizi zitakuwa mali ya Zanzibar na kuwa zitaleta maendeleo kwa kila familia, badala ya kung’olewa na wachache wenye maslahi binafsi.
Vilevile, kilimo na uvuvi vitasaidiwa na uwekezaji wa kisasa, kuhakikisha kila mshiriki anapata faida halisi ya kazi yake.
*Wasemavyo Wananchi*
Ali Abdalla Said wa Wete Pemba anasema kwa mara ya kwanza, wanaona kiongozi anayeweza kuwasaidia wakulima kuuza mazao yetu kwa bei nzuri.
Anasema pamoja na kuwa wanazalisha bidhaa nyingi za kilimo zenye uhitaji wa kupindukia lakini hawajawahi kuonja matunda Halisi ya bei za bidhaa zao.
Fatma Ngwali wa Makunduchi anasema Othman ni kiongozi ambae alihitajika miaka mingi kwa Wananchi wa Zanzibar na sasa ametokea.
Anasema kuna kila sababu Wananchi wote Unguja na Pemba kumchagua tena Kwa kura nyingi zaidi kuinusuru Zabzibar na kuijua maisha ya Wananchi.
“Othman anaelewa shida za walimu. Ahadi zake kuhusu mishahara na heshima yetu zinatupa matumaini.” – Juma Haji, Mwalimu wa Unguja.
“Ni jambo zuri kuona kiongozi anafikiria rasilimali za Zanzibar zinanufaisha wananchi wote, si wachache tu. Hii inatupa imani kuwa maisha yetu yatabadilika.” – Fatma Suleiman, Mkazi wa Mjini Unguja.
http://MAPOKEZI YA OTHMAN MASOUD UNGUJA NA PEMBA ISHARA YA RAIS MPYA AJAYE.