Moshi, Kilimanjaro
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa ndani ya Miaka mitano ijayo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali amedhamiria kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini kwa kuhakikisha utoshelevu wa dawa zote muhimu kwenye Vituo vya afya, kuongeza watumishi wa afya pamoja na Vifaa tiba kwenye Hospitali na Vituo vya afya nchini.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 wakati wa Mkutano wake wa Kampeni Moshi Mjini kwenye Viwanja vya Mashujaa akieleza kuwa katika kipindi chake cha kwanza cha serikali ya awamu ya sita wamefanikiwa kuongeza Upatikanaji wa dawa nchini hadi kufikia asilimia 86 na kazi hiyo itaendelea zaidi ikiwa atapewa ridhaa ya kuongoza serikali kupitia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amezungumzia pia maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi Mkoani Kilimanjaro, akisema kwasasa Hospitali hiyo inatoa huduma kwa wagonjwa mahututi, watoto wanaozaliwa kabla ya muda, usafishaji wa figo pamoja na vipimo vya kisasa, akikumbusha pia uzinduzi wa Jengo la Mama na Mtoto alioufanya katika kipindi chake cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
“Uwepo wa jengo lile limewezesha kuongeza idadi ya wanawake wanaojifungulia kwenye Hospitali mbalimbali tulizozijenga na akinamama wanaoitika kwenda Hospitali kwaajili ya huduma za uzazi na matibabu kwenye Mkoa huu imetoka 260,486 hadi 328,502 na kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kupunguza vifo vya akinamama wakati wa kujifungua na jitihada hizi zitaendelea zaidi ikiwa nitapewa ridhaa ya kuunda serikali.” Amesema Dkt. Samia.