Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi Oktoba 02, 2025 anatarajiwa kuendelea na Kampeni zake Mkoani Arusha akitarajiwa kuwa na Mkutano mmoja mkubwa wa Kampeni kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Dkt. Samia aliyeingia Mkoani Arusha jana Jumatano akitokea Mkoani Kilimanjaro na kufanya Mkutano mmoja kwenye Kituo cha mabasi Usa River Wilayani Arumeru amebainisha kuwa anarejea tena Mkoani Arusha kwa ujasiri kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana Mkoani hapa chini ya Uongozi wake wa serikali ya awamu ya sita iliyokaa madarakani katika kipindi cha miaka minne.
Ameeleza mafanikio makubwa katika kuimarika na kuongezeka kwa Upatikanaji wa dawa na Vifaa tiba, Kujenga Hospitali 2 za Wilaya za Karatu na Arusha Jiji, kuongeza Vituo vya afya kutoka 58 mwaka 2020 hadi 66 mwaka huu pamoja na ongezeko la Zahanati kutoka 312 hadi 350 sambamba na ukarabati na maboresho makubwa katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru, ikihusisha ujenzi wa majengo 4 ya huduma za dharura hospitalini hapo.
Serikali ya Dkt. Samia pia imewezesha ujenzi wa shule mpya 27 za sekondari na za Msingi 7 ndani ya Mkoa wa Arusha, kuimarika kwa huduma za maji safi na salama kutoka asilimia 69.2 mwaka 2020 hadi asilimia 77.3, kuongeza uzalishaji wa maji Jiji la Arusha kutoka lita Milioni 60 hadi Lita Milioni 200 kwa siku na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka saa 11 hadi 22 kwa siku kulikotokana na kukamilika kwa miradi mingi mipya.
Katika Nishati serikali ya Dkt. Samia imekamilisha uunganishaji wa umeme katika Mitaa yote 154, Vijiji vyote 395 pamoja na Vitongoji 1, 039 kati ya Vitongoji 1, 510, wakifanikiwa pia kujenga kituo cha kupooza umeme cha Lemugur (400 Kv) kwa lengo la kuunganisha gridi ya Taifa na Gridi ya Kenya sambamba na kuanza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya masoko, Vituo vya mabasi na maeneo ya maegesho la malori.
Dkt. Samia anajivunia pia kuongezeka kwa fursa za ajira kwenye sekta ya utalii, kuanzishwa kwa ranchi 4 za wanyamapori, Kukamilika kwa upanuzi wa kiwanja cha ndege Arusha ukijumuisha upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa njia ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami pamoja na kuanza utekelezaji wa mradi wa TACTIC katika Jiji la Arusha ukihusisha uboreshaji na ujenzi wa barabara za lami za Oljoro, Engo Sheraton na Olasiti ambazo zitaunganisha kituo kipya cha mabasi cha Bondeni City Jijini Arusha.