Home LOCAL DKT. SAMIA KUHITIMISHA MBIO ZA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU LEO

DKT. SAMIA KUHITIMISHA MBIO ZA KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU LEO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Oktoba 28, 2025 anatarajiwa kuhitimisha Kampeni zake za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kufanya Mkutano wa hadhara wa Kampeni kwenye Viwanja vya CCM Kirumba, Jijini Mwanza.

Dkt. Samia mwenye umri wa miaka 65, anaingia kwenye uchaguzi Mkuu wa Kesho Jumatano akiwa na rekodi ya kuwa Mwanamke wa kwanza kuidhinishwa na Chama Cha Mapinduzi kuwania nafasi hiyo, akiweka rekodi nyingine kabla ya kuwa Makamu wa Rais na Rais wa Kwanza mwanamke katika Historia ya Tanzania.

Dkt. Samia tayari ameizunguka Tanzania bara na Visiwani kwa siku 60, akifanya Mikutano ya hadhara ya kampeni zaidi ya 114 ambapo watu takribani Milioni 25.3 wamehudhuria Mikutano hiyo, Milioni 57.1 wakifuatilia kupitia Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, huku nambari za Mitandaoni zikionesha kuwa amefuatiliwa mara Milioni 164.9 kupitia majukwaa mbalimbali ya habari.

“Kwa ujumla amefanya Mikutano mikubwa viwanjani pia misafara yake imesimamishwa njiani mara kadhaa hivyo kulazimika kusimama na kuhutubia wananchi akiwa kwenye gari, mikutano ambayo yote imeandika rekodi ya kufuatiliwa zaidi katika historia.” Amenukuliwa akisema Katibu wa Itikadi, uenezi na mafunzo wa CCM Taifa Ndugu Kenani Laban Kihongosi.

Katika Ilani anayoinadi Dkt. Samia, ameahidi kuchochea Mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani, kuongeza fursa za ajira kwa Vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umaskini, kuboresha maisha ya watu na ustawi na kudumisha demokrasia na utawala bora kwa kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya na masuala mengineyo katika sekta mbalimbali.

Dkt. Samia katika kipindi chake cha miaka minne, mtindo wake wa uongozi, dhamira yake njema ya kushughulika na kero za wananchi pamoja na mageuzi mbalimbali ya kitaifa na Kimataifa hasa zaidi kutokana na Falsafa yake ya 4R, Dkt. Samia amefanikiwa kudumisha mshikamano na amani nchini, kurejesha uhusiano wa wafadhili pamoja na kuimarisha ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii, akifanikiwa pia kukamilisha miradi mingi ya Kimkakati, aliyoianzisha na aliyoachiwa na waasisi wake akiwemo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano.