Mgombea wa Nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 anatarajiwa kuendelea na Mikutano yake ya hadhara ya Kampeni za uchaguzi Mkuu wa baadaye Mwezi huu, akitua Moshi Mjini na Hai Mkoani Kilimanjaro na baadaye Mchana kubisha hodi Mkoani Arusha, akitarajiwa kuwa na Mkutano mdogo wa hadhara Wilayani Arumeru kwenye eneo la Usa River.
Dkt. Samia anatarajiwa kuwa na siku tatu za Kampeni Mkoani Arusha, ratiba ikionesha kuwa na Mkutano mkubwa wa hadhara Oktoba 02, 2025 kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha na baadaye Oktoba 03 akitarajiwa kuendelea na Mikutano yake Wilayani Monduli eneo la Mto wa Mbu na kuhitimisha Mikutano yake huko Karatu na kisha kuhamia kwenye Mkoa wa Manyara.
Dkt. Samia kwa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro anapotarajiwa kuwa na Mkutano kwenye Kata ya Bomang’ombe, Ilani ya Chama chake imeahidi ujenzi wa Vituo vya afya Kata za KIA, Nkwansira na Masama Kati, Ujenzi wa barabara za lami za Bomang’ombe Kikavuchini, Kwasadala- Longoi na Kwasadala- Mashua pamoja na sehemu ya barabara ya Bomang’ombe- Sanya Juu (Km25) sambamba na ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Vijiji vya Kiladeda, Metrum, Boloti, Rooside, Mwera, Kalali, Kikavu chini, Ismaili, Longoi, Mapacha na Mpendaroho.
Kwa Upande wa Moshi Mjini CCM imeahidi kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Moshi, Ujenzi wa barabara ya Kiwango cha lami ya Sokoine- (YMCA- KCMC, Kujenga ukumbi wa nje eneo la Shanty town, ujenzi wa stendi ya Ngangamfumuni, Ujenzi wa soko la Mbuyuni pamoja na ukamilishaji wa uwanja wa michezo unaojengwa Kata ya Majengo katikati ya Manispaa ya Moshi mkoani humo.