Home BUSINESS DKT. SAMIA AMEWEZESHA WATANZANIA KUNUFAIKA NA UTALII- MAKONDA

DKT. SAMIA AMEWEZESHA WATANZANIA KUNUFAIKA NA UTALII- MAKONDA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paul Christian Makonda amesema sekta ya Utalii katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imezalisha fursa nyingi za ajira kwa Vijana, kuchochea uchumi na kukuza pato la Taifa.

Amesema mwaka 2021 Watalii waliokuwa wanafika nchini walikuwa wakitumia Vyumba 5, 475 pekee huku Idadi ya watalii kutoka nje ya nchi wakiwa 788,000 pekee na baada ya Kuingia madarakani kwa Dkt. Samia pamoja na uongozaji wake wa filamu ya Royal Tour, imeleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo, Watanzania wengi wakiwa wanufaika wa matokeo ya jitihada hizo za kukuza na kutangaza utalii kupitia filamu na maboresho ya Sera ya Utalii ya Tanzania.

Makonda amebainisha hayo leo Oktoba 12, 2025 wakati wa Mkutano wa Kampeni za Dkt. Samia, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Wilayani Bukombe Mkoani Geita kwenye Viwanja vya shule ya Msingi Ushirombo, siku ya kwanza ya Kampeni za Dkt. Samis Mkoani humo.

“Ukiwaambia watu idadi ya watalii wanaofika nchini wanaweza wakahisi tu ni wageni na hawawahusu lakini hakuna mtalii au Mgeni nayetoka Ulaya anakuja na mchele, hakuna anayekuja na nyanya, hakuna anayekuja na kitanda ama walinzi. Maana yake hizi zote ni fursa ulizozitengeneza za ajira kwa Vijana wa Kitanzania.” Amekaririwa Mgombea huyo.

Makonda ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wote kuwa mabalozi wa Dkt. Samia na kumuombea kura katika maeneo mbalimbali nchini, akihimiza pia kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 ili kuwachagua Viongozi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ili kuwa na uhakika wa maendeleo na ustawi wao kwa miaka mitano ijayo.