Home BUSINESS DKT.SAMIA AMEFANIKIWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA, KUKUZA KIPATO CHA MTANZANIA – PROF....

DKT.SAMIA AMEFANIKIWA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA, KUKUZA KIPATO CHA MTANZANIA – PROF. KITILA MKUMBO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

MOSHI, KILIMANJARO 

Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanikiwa kupunguza gharama za maisha na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja kwa kutengeneza fursa za ajira na biashara nchini.

Profesa Mkumbo amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi wa moshi mjini katika mkutano wa Kampeni za Chama hicho, zilizofanyika leo Oktoba 1, 2025 Moshi Mjini.

Ameeleza kuwa wakati Mama Samia anaingia madarakani, kulikuwa na miradi 207 iliyosajiliwa, nakwamba hadi wakati huu tayari kuna miradi zaidi ya miradi 900 iliyosajiliwa, na ajira nyingi zimezalishwa, ambapo Serikali  imeendelea kuweka mazingira ya kupunguza gharama za maisha kwa watu wake ili kipato wanachopata kibaki mfukoni.

“kazi ya serikali ukiacha mambo ya ulinzi na usalama ni kutengeneza fursa kwenye maisha ya watu wake kwa kufungua fursa za wananchi kutengeneza ajira na biashara, na katika hili Mama Samia amefanikiwa sana.  Serikali ya Mama Samia imeweza kupeleka kwa wananchi moja kwa moja kwenye mifuko yao zaidi ya shilingi Trilioni 5.7, na wananchi Milioni 11 wamenufaika” ameeleza Prof. Mkumbo.

Amesema kuwa wananchi wamenufaika kupitia hatua muhimu nne ambazo ni mpango wa kaya maskini, ambapo alipeleka shilingi Bilioni 961 na watu Milioni 5 walinufaika. Aidha, sambamba na hilo, ni kupitia programu yake ya ruzuku za mbolea, iliyogharimu Shilingi Bilioni 693 na wananchi Milioni 2.2 wamenufaika moja kwa moja.

“Hatua nyingine ni kupitia programu ya elimu bila ada, Mama Samia amepeleka shilingi Trilioni 1.138 na wanafunzi zaidi ya Milioni 3 wamenufaika na hatua ya nne ni kupitia programu ya kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu ambapo Shilingi Trilioni 2.607 zimekwenda kwa wanafunzi na hizi ni fedha ambazo kwa namna moja ama nyingine ilibidi wazazi wazilipe lakini zimebaki mifukoni mwao na ni serikali ya Mama Samia iliyosaidia fedha hizi zibaki mifukoni mwa mwananchi ziongeze kipato na zipunguze gharama za maisha” ameongeza Prof. Kitila.