Mgombea mwenza katika kiti cha Urais kupitia CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa Serikali ijayo Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kuboresha sekta ya Uchukuzi mikoa ya kanda ya Kusini kwa kujenga meli mpya ya mizigo ikiwemo kupanua Kiwanja cha Ndege cha Mtwara, lengo ikiwa ni kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi kwa Wananchi.
Dkt.Nchimbi ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 02, 2025 akihutubia maelfu ya Wananchi wa Tandahimba waliofurika kumsikiliza wakati akinadi Sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030, katika muendelezo wa mikutano ya Kampeni za Urais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
“Nataka niwaambie ndugu zangu kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) moja ya ajenda zake muhimu ni kuhakikisha Sekta ya Uchukuzi inazidi kuimarika kwenye kanda hii ya kusini, ambapo baada ya Kuingia Madarakani tutajenga meli mpya ya Mizigo ambayo itasaidia kubeba Bidhaa kutoka hapa mtwara na kuzipeleka katika visiwa vya Comoro ili kuwa na Soko la Uhakika” amesema Dkt Nchimbi.
Aidha, Dkt.Nchimbi baada ya kuwahutubia Wananchi pia alipata fursa ya kuwanadi baadhi ya wagombea Ubunge wa mkoa huo,akiwemo mgombe Ubunge wa jimbo la Tandahimba,Ndugu Katani Ahmadi Katani pamoja na Madiwani.