
Chama cha ACT Wazalendo kimeahidi kuja na mpango kabambe utakaohakikisha unasafisha mji wa kigoma kwa kujenga barabara za ndani, kufukia makorongo na kutengeneza mifereji, kitakapofanikiwa kuongoza manispaa ya kigoma ujiji baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Kauli hiyo imetolewa jana, Oktoba 23, 2025 na mgombea ubunge jimbo la kigoma mjini kwa tiketi ya chama hicho, Zitto Kabwe wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Mwanga Kaskazini, alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa chama katika kata hiyo, Wakili Mubanga.
Zitto alisema chama chake kitakwenda kuendeleza rekodi ya ujenzi wa miundombinu katika manispaa hiyo kama kilivyofanya kati ya mwaka 2015 hadi 2020 wakati kikiongoza manisapaa hiyo.
“Hakuna wakati mji wetu wa kigoma ulishughulika na miundombinu kama wakati ambao sisi tunaongoza manispaa chini ya Meya wetu Ruhava na Naibu Meya Luga na madiwani wetu, ndio kipindi tumesimamia miradi mikubwa ya maendeleo”, alisema Zitto
Alisema dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha kinafanyia kazi ahadi zake ambapo huziweka katika maandishi na kugawa vipeperushi kwa wananchi ili wabaki na ushahidi endapo hakitatekeleza ahadi hizo.
“Ahadi namba sita kwenye kipeperushi chetu hiki tulichowagawia na naomba mkitunze kama ushahidi, inahusu kusafisha mji wetu wa kigoma ili uwe miongoni mwa miji bora katika nchi yetu”, aliongeza Zitto
Aliongeza chama hicho kikipata madaraka hakiendi kuanza mwanzo kutekeleza ahadi zake kwa kuwa tayari mipango ya maendeleo katika manisapaa hiyo kiliianzisha kabla ya chama cha CCM kupokea kijiti mwaka 2020-2025.
 
  
 
 
  
            
