Akiwa Uyui Mkoani Tabora leo Alhamisi Septemba 11, 2025 kwenye Mkutano wa Kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi chake cha kwanza kama Rais wa Tanzania miradi 15 ya Maji ilitekelezwa Wilayani humo na kufanikisha upatikanaji wa maji kwa asilimia 67 Wilayani humo.
Mbele ya maelfu ya wananchi waliofika kumlaki na kumsikiliza kwenye siku yake ya pili ya kampeni Mkoani Taboraz Dkt. Samia pia amesema kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria utakwenda kuongeza idadi zaidi ya upatikanaji wa maji Wilayani humo, akisema serikali yake imepanga kujenga Tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita Milioni 1 kwenye Kata ya Ilolangulu ili kuhudumia wananchi wa Kata hiyo na Kata za Kalola, Isila, Ndono na Mabana.
Dkt. Samia pia kwa kutambua changamoto ya maji Wilayani humo, ameahidi ikiwa atapata ridhaa tena ya Kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo atahakikisha anakamilisha miradi ya maji ya Kigwa, Bwawa la Igombe, na Kizengi, akisema dhamira yake ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi ya uhakika na salama.
Dkt. Samia kadhalika amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26 serikali ya awamu ya sita pia imetenga fedha kwaajili ya ujenzi wa daraja la mto Loya Wilayani Uyui ambapo tayari usanifu umekamilika pamoja na michoro ya daraja hilo na kulitaja daraja hilo kama muarobaini wa changamoto waliyokuwa wakiipitia wananchi wa eneo hilo hasa nyakati za masika.