Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba kura za ushindi Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura hapo Oktoba 29, 2025, akiwashukuru kwa ushirikiano wao katika kipindi chake cha awamu ya kwanza na kuwaomba kuendelea kushirikiana naye katika kutimiza dhamira yake njema ya kuwaletea Watanzania wote maendeleo.
“Maendeleo ni hatua na hakuna awamu itakayomaliza maendeleo tukasema kwamba hapa tumefikia mwisho hatuhitaji kingine, tutafanya kwa kadri tutakavyojaliwa na Mungu na wengine wataendeleza pale tutakapoishia kutokana na mahitaji kuongezeka na kuzaliana kwetu. Ni wajibu wetu kuendelea kutumikia mahitaji ya wananchi na tunashukuru kwa ushirikiano mliotupatia kwa miaka mitano iliyopita na tunaomba ushirikiano huo ili tukafanye makubwa zaidi.” Amekaririwa akisema Dkt. Samia.
Kulingana na Dkt. Samia, Ahadi na dhamira kuu kwa Zanzibar ikiwa atapewa ridhaa ya kuongoza Tanzania itakuwa ni kukuza uchumi jumuishi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Wazanzibar wote, akiahidi fursa za ajira kwa vijana 350,000, kuongeza pato la Mtanzania kwa Dola za Marekani 1, 880 kwa mwaka kufikia mwaka 2030 kutoka Dola 1,210 za sasa pamoja na kuongeza thamani ya biashara kwa Zanzibar (trade Value) na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa.
Dkt. Samia pia kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 anayotarajiwa kuendelea kuinadi kesho Septemba 20, 2025 Kisiwani Pemba, ameahidi pia kuendeleza programu za kujenga umahiri kwa wahitimu, kulinda fursa za ajira kwa wazawa, kuandaa programu za kuwavutia wawekezaji na sekta binafsi kuajiri Vijana, kando ya uendelezaji na uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, malazi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafiri, usafirishaji na mawasiliano Visiwani Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi kinachoongozwa na Dkt. Samia akiwa ndiye Mwenyekiti wake Taifa kadhalika kimewaahidi Wazanzibar kuanzisha Mji wa kidigitali wa Fumba na kuiunganisha Zanzibar na mkonga wa Kimataifa, kupanua matumizi ya maudhui ya kidigitali na bidhaa za kitamaduni ili kuongeza mvuto jwa watalii na kukuza uchumi wa kidigitali, kuanzisha usafiri wa taksi za baharini, pamoja na kujenga bohari ya Gesi yenye ujazo wa tani 1,500.
http://TUPENI USHIRIKIANO TUENDELEE KUSHUGHULIKA NA MAHITAJI YENU- DKT. SAMIA