Home BUSINESS TUMETUMIA SH. BILIONI 726 KUGAWA MBOLEA NA PEMBEJEO NCHI NZIMA

TUMETUMIA SH. BILIONI 726 KUGAWA MBOLEA NA PEMBEJEO NCHI NZIMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tangu kuanza kwa Mpango wa serikali wa kutoa ruzuku za mbolea pamoja na pembejezo za Kilimo mwaka 2021/22, serikali imetumia takribani Bilioni 726 kwaajili ya kunufaisha wakulima wa Tanzania.

Akiomba kura kwa mamia ya wananchi wa Mtwara Mjini leo Septemba 26, 2025 kwenye Viwanja vya Nanenane Mkoani Mtwara, Dkt. Samia ameeleza dhamira yake ikiwa wananchi wataendelea kukipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi ni kuendelea kuongeza kiwango hicho cha ruzuku ili kukuza uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima.

“Tunatumia shilingi Bilioni 152 kila mwaka pesa ambayo ingetoka mfukoni kwa Mkulima lakini tumeibakisha mifukoni kwao na serikali tunagawa kwa ruzuku ya nusu bei na pembejeo nyingine ni bure kabisa kama salfa, dawa za kuulia wadudu na blight na tunafanya hivyo kwasababu tumedhamiria kukuza kilimo na uzalishaji wa Korosho na kwa hakika uzalishaji tumeuona ikiwemo kwenye zao la korosho kutoka tani 118, 811 mwaka 2020/21 zikiwa na thamani ya Bilioni 265 na leo mwaka 2024/25 tunazungumzia uzalishaji wa tani 330, 505 zikiuzwa shilingi Trilioni moja na Bilioni 900.” Amesema Dkt. Samia.

Katika hatua nyingine Dkt. Samia ameahidi kukamilisha miradi ya Umeme Mkoani Mtwara ikiwemo mradi wa kuziunganisha Mtwara na Lindi kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa kutokea Songea, Tunduru mpaka Masasi pamoja na ujenzi wa vituo vya kupooza umeme Tunduru na Masasi ili kuhakikisha Mtwara inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.