Home LOCAL TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA KWA AWAMU YA PILI YA UDAHILI 2025/2026

TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA KWA AWAMU YA PILI YA UDAHILI 2025/2026

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetangaza kufunguliwa kwa Awamu ya pili ya udahili wa Shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kuanzia leo Septemba 3 hadi 21, 2025, na kuwaasa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au kutopata nafasi katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali watumie fursa hiyo.

Akiongea katika Mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema kuwa hatua ya kufunguliwa kwa dirisha hilo imefuatia baada ya kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya udahili wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026, na kwamba majina ya waliodahiliwa katika awamu hiyo yatatangazwa na vyuo husika.

Amesema, Tume inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi, nakwamba waombaji udahili na vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili wa Aawamu ya pili kama inavyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyoko katika tovuti ya TCU – www.tcu.go.tz

Akizungumzia kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya udahili, Profesa Kihampa amesema kuwa jumla ya waombaji 146,879 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza, ambapo jumla ya programu 894 zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 856 mwaka 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la programu 38 za masomo.

Kwa upande wa nafasi za udahili, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 205,652 ikilinganishwa na nafasi 198,986 mwaka uliopita. “Hili ni ongezeko la nafasi 6,666 sawa na asilimia 3.3 katika programu za Shahada ya Kwanza,” amesema Profesa Kihampa.

Ameongeza kuwa, katika Awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 116,596 sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote walioomba udahili wamedahiliwa kwenye vyuo walivyoomba, ambapo idadi ya waombaji wa udahili na watakaodahiliwa inatarajiwa kuongezeka katika awamu ya pili ya udahili.

Amesisitiza kuwa, waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo Septemba 3, hadi Septemba 21, 2025, na kwamba, uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

“Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kuithibitisha katika chuo husika” amesisitiza.