Na: Hughes Dugilo, Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha Afya za watanzania zinaendelea kulindwa, Seikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), linaimarisha mikakati yake mbalimbali ya kuboresha huduma na kuwezesha Biashara, kwa kuinua uchumi wa viwanda, ili vizalishe bidhaa zenye ubora na salama, utakaokidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, katika kikao kazi kati ya Shirika hilo, pamoja na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Septemba 18,2025, jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Dkt. Katunzi amesema, ili kulifanikisha hilo TBS imetenga shilingi milioni 350 kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo na wa kati nchini, kwa kuwasaidia kuhakikisha bidhaa zao zinapata uthibitisho wa ubora.
“TBS itaendelea kushirikiana na watendaji wa halmashauri kote nchini, ili kuwatambua wajasiriamali wenye bidhaa zilizokidhi viwango lakini wameshindwa kupata uthibitisho wa ubora kutokana na changamoto za kifedha” amesema Dkt. Katunzi.
Awali akizungumza katika Mkutano huo, Dkt, katunzi ameweka bayana mafanikio ya Shirika hilo, yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Mheshiwa Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan, na kusema kuwa mafanikio hayo yameendelea kutimiza azma yao katika masuala mbalimbali, na kukidhi matamanio ya wadau na Taifa kwa ujumla.
Amesema, pamoja na mambo mengine, Shirika limetanua huduma zake katika mikoa ya kimkakati, Dodoma na Mwanza kwa kuanzisha ujenzi wa maabara za kisasa utakaogharimu jumla ya shilingi 36,802,360,422.39, ambapo Shilingi 24,723,478,765.48 kwa Dodoma, na Shilingi 12,078,881,656.91 katika mkoa wa Mwanza.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa Dodoma Maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya kati ambayo ni Dodoma, Singida, na Tabora, pamoja na mikoa mingine ya karibu, huku maara za Mwanza zitahudumia mikoa sita ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.