Home BUSINESS NIA YETU NI KUING’ARISHA BUHIGWE KWA UMEME WA UHAKIKA

NIA YETU NI KUING’ARISHA BUHIGWE KWA UMEME WA UHAKIKA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ikiwa atachaguliwa kuongoza serikali kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Serikali yake itahakikisha Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma inakuwa na umeme wa kutosha, ili kuvutia uwekezaji wa viwanda na biashara Wilayani humo.

Dkt. Samia ameyasema hayo alipowahutubia wananchi wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika leo Jumamosi Septemba 13, 2025, katika wilaya hiyo, ambapo amesema serikali yake itatekeleza mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji ya Mto Malagarasi utakaozalisha megawati 46 zitakazosambazwa kwenye Wilaya hiyo.

“Nia yetu ni kuifanya Buhigwe ing’are kwa umeme wa kutosha ili tuweze kuweka uwekezaji wa viwanda.

“Nimeambiwa vijana wa Buhigwe ni wakulima wazuri wa tangawizi, tunataka iongezewe thamani kwa kujenga kiwanda hapa Buhigwe.

“Tunamuomba Mwenyenzi Mungu atujalie afya, furaha na uhai wana Buhigwe na Watanzania wote ikifika tarehe 29 mwezi wa kumi tuamke mapema kwa wingi wetu kama tulivyo hapa tuende kwenye vituo vya kupigia kura tukamchague Rais, Mbunge na diwani wa Chama Cha Mapinduzi. Ndugu zangu kwa heshima ninaombeni kura zenu.” Amesisitiza Dkt. Samia.

Aidha, Dkt. Samia ameeleza mpango wake wa kuanza majaribio ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote mara baada ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao, akisema serikali yake itagharamia pia matibabu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kulipia bima hizo za afya.