Home LOCAL NHC YAKABIDHI MSAADA KWA WATU WENYE ULEMAVU UBUNGO

NHC YAKABIDHI MSAADA KWA WATU WENYE ULEMAVU UBUNGO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kupitia kwa Afisa wake Mkuu wa Habari, Yahya Charahani, limekabidhi msaada wa vifaa vya kusaidia watu wenye ulemavu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Msaada huo umejumuisha magongo ya kutembelea (crutches), baiskeli za walemavu, na vifaa vingine vya kusaidia watu wenye uhitaji maalum kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Yahya Charahani alisema:

> “Tumefika hapa leo kwa niaba ya Shirika la Nyumba la Taifa kuonyesha mshikamano wetu na watu wenye ulemavu. Tunatambua changamoto wanazopitia, na msaada huu ni sehemu ndogo ya mchango wetu kwa jamii ambayo sisi pia ni sehemu yake.”

Aliongeza kuwa shirika hilo limeweka sera za kijamii zinazolenga kusaidia makundi maalum katika nyanja za elimu, majanga, na ustawi wa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayejua lini maisha yanaweza kubadilika.

> “Sisi sote ni walemavu watarajiwa. Leo hii ni wao, kesho inaweza kuwa mimi au wewe. Tunaposaidia, hatufanyi hivyo kwa sababu tuna ziada, bali kwa sababu tunatambua utu wa kila mmoja,” alisisitiza Charahani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Ubungo, Athmani Hassani Sembe, alishukuru kwa niaba ya wanachama wake:

> “Tunashukuru sana kwa moyo wa upendo mlioonyesha. Wanachama wetu watafurahia sana msaada huu, hasa wale ambao walikuwa hawana vifaa vya kutembelea. Huu ni msaada unaogusa maisha moja kwa moja.”

Naye Naibu Katibu wa chama hicho, Saidi Mbogo, alieleza kuwa msaada huo sio tu umeleta matumaini, bali pia umeonyesha kuwa bado kuna mashirika yanayowajali watu wenye ulemavu:
> “Ni mashirika machache sana yenye moyo kama huu. Tunawashukuru sana NHC. Vifaa hivi ni kama miguu ya tatu kwa wengi wetu – vinaongeza uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii.”

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho, maafisa wa NHC na wanahabari, huku ikihitimishwa kwa maombi na pongezi kwa mshikamano ulioonyeshwa baina ya sekta ya umma na jamii.