

Dar es Salaam
Tume ya ushindani Tanzania Bara -FCC imeingia mashirikiano na Tume ya ushindani halali wa biashara Zanzibar -ZFCC yatakayojielekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa feki.
Akizungumza muda mfupi baada ya kushuhudia mashirikiano hayo Jijini Dar es salaam Katibu Mkuu wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah amezielekeza taasisi hizo kuyafanyia kazi yale yote yaliyokusudiwa ili kuongeza ufanisi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Amesema makubaliano hayo yanapaswa kujikita katika kutatua changamoto za ushindani ikiwemo kwenye sekta ya biashara na viwanda lengo ni kuleta uhimilivu toshelezi wa uchumi.
“Kwanza, FCC na ZFCC zinapaswa kuteua watu au timu maalum kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya. Pia, ndani ya kipindi cha miezi mitatu—au hata chini ya mwezi mmoja—ni muhimu kutengeneza nyaraka kama ‘roadmap’ au ‘plan of action’ zitakazotuongoza katika utekelezaji,” alisema Dkt. Hashil.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupanga muda wa utekelezaji wa kila jukumu. “Kitu kisipopangiwa muda mara nyingi hakitekelezeki. Tunapaswa kujua tunatekeleza nini na kwa muda gani, ili tukifika wakati husika tuweze kujitathmini,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara ya mshikamano wa kitasisi na dhamira ya pamoja ya kulinda ushindani wa haki na maslahi ya walaji katika pande zote za Muungano.
“Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza nguvu na uwezo wa pamoja kukabiliana na changamoto za ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji, ambazo mara nyingi huathiri Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Bi. Aliyah Juma, alisema tume yao ipo tayari kushirikiana kwa karibu na FCC katika utekelezaji wa makubaliano hayo.
“Tunalenga kushughulikia changamoto zote zilizopo sokoni kwa pamoja ili kulinda ushindani wenye tija na haki kwa pande zote. Sisi kama ZFCC tuko bega kwa bega kuhakikisha kile kilicho kwenye makubaliano kinatekelezwa kwa weledi na ufanisi,” alisema.




