Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Kaliua Mkoani Tabora leo Septemba 11, 2025 kwenye Mkutano wa Kampeni, amesema Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza kuhamasisha upimaji wa viwanja kwenye eneo la Kasungu, Ufukutwa na Ushokola Wilayani Kaliua na kumilikishwa viwanja kwa wananchi kwaajili ya makazi na biashara.
Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na ahadi za Chama Cha Mapinduzi kuelekea mwaka 2030 ikiwa Chama hicho kitachaguliwa kuongoza serikali kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema serikali za Mkoa na Serikali kuu watawajibika kuhakikisha ardhi hizo zinaendelezwa kwa manufaa.
Amebainisha pia kwamba serikali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM itawajibika kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kwa kuhakikisha ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa watapata ridhaa ya kuongoza, barabara za Wilaya hiyo zinajengwa kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Banyanga, Masudi- Silimu- Msufini- Kisamvu mpaka Machibya 1 pamoja na barabara ya KKKT- Kibonde A- Osterbay.
Aidha Dkt. Samia pia ameahidi ku,ifunga barabara mpya za Seleli- Muhalaja na barabara ya Ulyankulu.
Ameahidi pia kujenga barabara za viwango vya changarawe ili ziweze kupitika nyakati zote za msimu ikiwemo barabara ya King’wang’oko- Usonga, Taba- Imara- Keza- Ichemba- Ngwande, Sasu- King’wang’oko- seleli, Mpanda Mlowoka- Mhalaja, Uyoha- Msungwa- Ulyankulu, Ufukutwa- Tuombe Mungu- Mkuyuni na barabara ya Keza- Igombe.