Home LOCAL DKT. SAMIA: TUTAENDELEA KULETA MBOLEA YA RUZUKU KWA WAKULIMA, WAFUGAJI KIGOMA

DKT. SAMIA: TUTAENDELEA KULETA MBOLEA YA RUZUKU KWA WAKULIMA, WAFUGAJI KIGOMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo, Mbolea, chanjo pamoja na huduma bora za ugani kwa wakulima na wafugaji ikiwa atachaguliwa kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Dkt. Samia ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 13, 2025, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kazuramimba, Uvinza Mkoani Kigoma wakati wa Kampeni zake kuelekea uchaguzi Mkuu, huku akiwapongeza akinamama wa Wilaya hiyo kwa kujishughulisha vyema na shughuli za kilimo.

Aidha. ameahidi pia kujenga vibanda kwenye masoko ya Wilaya hiyo, ili kuwasaidia wananchi wa eneo hilo kupata sehemu ya kuuzia mazao na bidhaa zao za kilimo.

“Kwa kuwa akinamama ni wazalishaji wazuri wa mazao na wanakosa soko, nimeambiwa wanauza biashara zao pembeni mwa barabara, niwaahidi akinamama kuwa mimi nikishirikiana na wabunge wa viti maalumu tutawajengea mabanda muweze kuuza bidhaa zenu kwa raha sehemu yenye kivuli.” Amesema Dkt. Samia.

Dkt Samia Suluhu Hassan ameanza mikutano yake ya kampeni Mkoani Kigoma akitokea Mkoani Tabora ambapo pamoja na mengine anatumia mikutano hiyo kueleza mafanikio ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita pamoja na ahadi zake mbalimbali kuelekea mwaka 2030.