Home LOCAL DKT. SAMIA KUZUNGUMZA NA WANANCHI AKIHITIMISHA KAMPENI ZA CCM TABORA LEO

DKT. SAMIA KUZUNGUMZA NA WANANCHI AKIHITIMISHA KAMPENI ZA CCM TABORA LEO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Ijumaa Septemba 12, 2025 anahitimisha mikutano yake ya kampeni Mkoani Tabora, ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho katika mkoa huo.

Dkt. Samia anatarajiwa kuwa na mkutano mkubwa wa kampeni utakaofanyika Tabora Mjini kabla ya kuelekea katika mikoa mingine nchini.

Awali akiwa Kaliua Mkoani humo, Dkt. Samia aliahidi kuendeleza ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za Ukumbi, Siganga, Kashishi, Ugunga na Ichemba, kukamilisha ujenzi wa zahanati nane za Imalaupina, Ushokola, Igombe, Sitini, Mnange, Keza, Ikonongo, Igwisi na Mwahajala, kujenga barabara ya Banyanga, Masudi- Silimu- Misufini, Kisamvu, Machibya 1, Kibonde R, Oysterbay na KKKT kwa kiwango cha lami, pamoja na ujenzi wa mabwawa na skimu za umwagiliaji za Konane, Igombe, Mnange, Nimbula na Igwisi sambamba na uwezeshaji mradi wa BBT kwa Vijana wa Wilaya ya Kaliua.

Kwa Urambo ikiwa atachaguliwa kwenye Uchaguzi mkuu unaotarajiwa hapo Oktoba 29, 2025, Dkt. Samia ameahidi kujenga barabara ya Emirates- Mnyonge- Usoke- Urambo- Ukwanga- Igunguli- Milambo, Urambo- Kangeme- Izimbili- Mabama- Tebela- Uwima, Usoke- Kindwa kwa kiwango cha lami, ujenzi wa shule mpya 12 za msingi na sekondari pamoja na ujenzi wa soko la mazao na skimu za umwagiliaji Uyogo na Izimbili.

Katika wilaya ya Uyui, Dkt. Samia ameahidi ndani ya siku zake 100 ikiwa atachaguliwa ataajiri watumishi 5, 000 katika sekta ya afya, watumishi 7,000 katika sekta ya elimu nchi nzima, ujenzi wa tanki kubwa la maji la kujifadhi lita Milioni 1 ya maji kutoka ziwa Viktoria ili kuhudumia Kata 5 za Ilolangulu, Kalola, Isila, Dono na Mabama pamoja na ujenzi wa daraja la mto Loya kando ya masuala mengineyo.

Katika Ilani ya CCM ya 2025/30, Chama hicho kwa Tabora Manispaa wameahidi umaliziaji wa hospitali ya Manispaa, kituo cha afya Itetemia, Misha na Tumbi pamoja na zahanati ya Kapunze, ununuzi wa vifaa tiba, ujenzi wa shule mpya nne, mabweni 16, nyumba za waalimu 46, ukamilishaji barabara ya Tabora- Ipole-Koga- Mpanda (Km202), pamoja na ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege Tabora na kupanga, kupima na kumilikisha maeneo 300 yanayomilikiwa na Halmashauri pamoja na ununuzi wa kifaa cha upimaji ardhi (GPS RTK).