Home LOCAL DKT. SAMIA KUUNGURUMA KIGOMA MJINI AKINADI SERA KWA WANANCHI

DKT. SAMIA KUUNGURUMA KIGOMA MJINI AKINADI SERA KWA WANANCHI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Kufanya Mkutano Mkubwa wa hadhara,-kunadi sera zake na kuwanadi Wagombea Ubunge wa Majimbo yote ya Kigoma_

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumapili Septemba 14, 2025 anatarajiwa kuwa na Mkutano mkubwa wa hadhara wa Kampeni Kigoma Mjini Mkoani Kigoma akitokea kwenye Wilaya za Kasulu, Uvinza na Buhigwe katika muendelezo wa kampeni zake kwenye Mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Katika Mkutano huo Dkt. Samia anatarajiwa kunadi sera na ahadi zake kuelekea 2030 pamoja na mafanikio aliyoyapata kwenye miaka minne ya serikali ya awamu ya sita pamoja na kuwanadi wagombea Ubunge wa Majimbo yote ya Mkoa huo wa Kigoma.

Awali kwenye Wilaya za awali alizopita kuomba kura mkoani humo, Dkt. Samia ameahidi kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa Kitovu cha biashara kwa nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Ukanda huo wa Ziwa Tanganyika, akiahidi ikiwa atachaguliwa ataendelea kuboresha miundombinu, kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuendelea kuvutia zaidi wawekezaji kuwekeza katika Mkoa huo.

“SGR ni mradi wa Kitaifa na bahati nzuri Kigoma mmebahatika, mtakuwa na vituo Vingi zaidi kuliko Mikoa mingine lakini kwasababu reli hii inamalizikia Kigoma Fursa kubwa sana za kibiashara zitakuwa hapa Kigoma. Lengo ni kuufungua Mkoa huu kwahiyo ndugu zangu wa Kigoma changamkieni fursa hizo kwa kufanya biashara na nchi jirani na hata ndani ya Tanzania.” Amesema Dkt. Samia.

Akizungumzia suala la umeme Dkt. Samia amesema Mkoa huo bado unakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme inayosababishwa na kuwa mbali na vyanzo vya kuzalisha umeme, hivyo serikali yake ijayo itazalisha umeme wa Megawati 49.5 kutoka kwenye mto Malagarasi kwaajili ya baadhi ya maeneo ya Mkoa huo.

Katika kufungua njia za kibiashara Mkoani humo kuelekea nchi jirani, serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia inatekeleza mradi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Tabora hadi Kigoma hatua itakayorahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar Es Salaam, mradi ukitarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kupunguza gharama za biashara na kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo, uvuvi na viwanda Mkoani humo huku pia ukitoa ajira kwa Vijana.

Kwa Mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Mkoa wa Kigoma una jumla ya wakazi 2, 470, 967, wanaume wakiwa 1, 186, 833 na wanawake ni 1, 284, 134, idadi inayoufanya Mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa yenye ongezeko kubwa la watu na hivyo kuongeza uhitaji wa huduma za kijamii, miundombinu na fursa za kiuchumi.