Home BUSINESS DKT.SAMIA: KIGOMA SASA SIO MWISHO WA RELI, NI KITOVU CHA BIASHARA NA...

DKT.SAMIA: KIGOMA SASA SIO MWISHO WA RELI, NI KITOVU CHA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu katika mkoa wa Kigoma, sambamba na kuufungua mkoa huo kupitia njia za reli, anga, barabara na usafiri wa majini, ili kutimiza adhma ya kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika, kutokana na mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa ya kimkakati nchini,

Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo kwenye viwanja vya Katosho, wakati wa Mkutano wake wa kampeni uliofanika leo Jumapili Septemba 14, 2025 Mjini Kigoma, ambapo amesema kuwa katika kutekeleza hayo, serikali yake inaendelea na ukarabati wa Viwanja 14 vya ndege, akisisitiza kuwa Kigoma haitokuwa tena mwisho wa reli kwani Ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR itakayofika Kigoma itaenda pia kwenye Mataifa ya Burundi na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Kigoma hii ya sasa sio mwisho wa reli, bali ni kitovu cha biashara na maendeleo. Na ili kufikia lengo hilo kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ambao ndio muhimili mkubwa wa kukuza uchumi, tumejidhatiti kuunganisha Mkoa huu kwa njia zote ikiwemo barabara, anga, reli na njia ya maji na tayari maboresho ya uwanja ndege yanaendelea, Njia tayari imeanza kutumika na jengo la abiria linaendelea kujengwa.” amesema Dkt. Samia.

Ameahidi pia kusimamia upatikanaji wa umeme wa Uhakika mkoani humo kwa kujenga kituo kipya cha kupokea na kupooza umeme pamoja na mradi wa uzalishaji wa umeme kupitia mto Malagarasi ili kuvutia zaidi uwekezaji wa Viwanda Mkoani humo pamoja na kuwezesha utekelezaji wa kongani ya viwanda katika mkoa huo, nakwamba viwanda hivyo vitasaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo Tangawizi na chikichi, kwani serikali yake imedhamiria kukuza uzalishaji wa mafuta ya kupikia kulingana na mahitaji, ili kuondokana na uagizaji wa mafuta hayo nje ya nchi.

Dkt. Samia pia amesema kando ya ujenzi wa reli hiyo, Serikali pia itafanya maboresho ya reli ya zamani ya MGR, wakinunua vichwa vipya 3 vya treni, Mabehewa mapya 22 ya abiria na 44 ya mizigo, huku ukifanyika ukarabati wa mabehewa 350 ya mizigo, na 33 ya abiria sambamba na mabehewa maalumu yenye kuhifadhi baridi kwaajili ya usafirishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda.

Dkt. Samia pia amezungumzia maboresho ya sheria na kanuni kuhusu waendeshaji wa huduma za reli kwa kuruhusu waendeshaji binafsi kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji kwenye miundombinu ya reli iliyowekwa na serikali, kama sehemu ya kuendelea kuongeza huduma bora kwenye usafiri wa reli nchini.