
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameendelea na kampeni zake za Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, akiahidi kuendeleza miradi yote mikubwa inayolenga kuinua ustawi wa wananchi.
Katika sekta ya afya, Dkt. Samia ameahidi kuwa itakuwa atapata nafasi, Serikali yake itakamilisha ujenzi wa vituo vitatu vipya vya afya katika maeneo ya Mtoa, Mwandegembe na Irungu, hatua ambayo itaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Iramba.
Kuhusu elimu, Mgombea huyo wa Urais ameeleza kuwa Serikali yake ijayo imekamilisha ujenzi wa shule mpya ya Amali pamoja na Shule ya Sekondari ya Mbelekese, ili kuongeza nafasi za wanafunzi kuendelea na masomo kwa mazingira bora na yenye hadhi.
Kwa upande wa maji, Dkt. Samia amesema Serikali imetekeleza ujenzi wa tenki kubwa la maji Kizonzo lenye ujazo wa lita 300,000, na pia itaendeleza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, ili kuhakikisha wananchi wa Iramba wanapata maji safi na salama kwa uhakika.
Vilevile, kupitia sekta ya madini, Serikali imeanzisha soko la uuzaji wa dhahabu, litakalowawezesha wachimbaji wadogo kupata masoko yenye uhakika na kuongeza kipato cha wananchi.





