

SAME KILIMANJARO
Mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama cha CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kumaliza tatizo la vifo vya kinamama na watoto vinavyotokana na changamoto ya uzazi, endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa kuiongoza serikali katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Mwaka huu.
Dkt. Samia ameyasema hayo alipozungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wake wa kampeni za Chama hicho, uliofanyika leo wilayani Same, Kilimanjaro, ambapo ameeleza kuwa katika Wilaya hiyo, tayari serikali imejenga vituo sita, nakwamba sasa inakamilisha vituo vingine vitatu vya afya na Zahanati tano katika wilaya hiyo.
“lakini katika siku za mbele huko tunakwenda kujenga vituo vingine vya afya wenye Kata za Vudee, Mshewa na Makanya.
“Mwaka 2010 nilipoanza kampeni kwa mara ya kwanza kama Mgombea mwenza kituo cha kwanza kwenye Kampeni zile ilikuwa Wilaya ya Same na nilienda kwenye Zahanati moja pale Hedaru na kilichonisikitisha ni kuona huduma za kinamama wajawazito kujifungua pale lakini hali niliyoiona haikunifurahisha hata kidogo. Pamoja na kwamba nilikuwa Mgombea mwenza niliweka nia ya kurekebisha hali ile kwa Tanzania nzima. Leo namshikuru Mungu nimeweza kuirekebisha hali ile na tutaendelea kujenga Hospitali za Wilaya, Vituo vua afya vyenye zana kamili za matibabu, dawa na watumishi.
“Nilikuwa Pwani, Chalinze na Bagamoyo hawana taarifa ya mwanamke aliyefariki wakati wa kujifungua kwa mwaka mzima huu na hilo ndilo lengo letu, kufa kupo tutakufa lakini kujifungua isiwe sababu, kuleta maisha mapya isiwe sababu. Kwahiyo tutajitahidi kueneza vituo vya afya, Hospitali za Wilaya zenye vitendea kazi kamili kwa Tanzania nzima” amesema Dkt. Samia.





