
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema katika kulinda maslahi ya wakulima wa Mbaazi na dengu nchini Tanzania, Serikali ya awamu ya sita ilishaanza mazungumzo na Soko kubwa la mazao hayo nchini India ili kuweza kununua mazao hayo kwa bei nzuri licha ya soko la dunia kushuka kutokana na wingi wa mavuno.
Dkt Samia ameyaeleza hayo wakati wa Mkutano wake wa Kampeni Wilayani Iramba Mkoani Singida akiwa njiani kuelekea Mkoani Tabora leo Jumatano Septemba 10, 2025, akisema kuwa zao la Mbaazi na dengu halitoshuka zaidi ya asilimia 60 ya bei ya soko la dunia.
Dkt. Samia pia ameeleza mafanikio ya mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia soko la mtandaoni kwa mazao ya dengu, mbaazi, choroko na ufuta, akisema mfumo huo umeongeza uwazi na kuwakutanisha moja kwa moja wakulima na wanunuzi na hivyo kuepusha ulanguzi uliokuwa ukifanywa na madalali wasiokuwa waaminifu.
Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba kura wananchi wa Iramba, akiwashukuru watanzania kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano yake ya kampeni.
“CCM ina mipango mikubwa ya kuchochea maendeleo ya nchi yetu hivyo nitoe rai kwa kila mwananchi kujitokeza tarehe 29 Oktoba na kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwasababu ya wingi huu tunaokuja kwenye mikutano, wingi huu huu unatarajiwa kwenye masanduku ya kura sasa haitapendeza uwanjani tunakuja kwa wingi hivi Mashaallah ili kuonesha imani kwa Chama chetu basi mkaoneshe imani hii hii pia kwenye sanduku la kura.” Amesisitiza Dkt. Samia.





