_Barabara hiyo ya lami kupunguza foleni na kuifungua zaidi Tabora Mjini_
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake ikiwa atachaguliwa kuongoza kwa miaka mitano ijayo pamoja na mambo mengine atahakikisha anaendelea kujenga mitandao ya barabara za lami nchini pamoja na za changarawe ili kuruhusu barabara za Mijini na Vijijini kuweza kupitia muda wote nchini.
Dkt. Samia ameeleza hayo leo Ijumaa Septemba 12, 2025 Mkoani Tabora wakati wa Mkutano wake wa Kampeni Tabora Mjini kwenye Uwanja wa Ipuli akisema kwa mwaka 2025/26 serikali ya awamu ya sita pia imeongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Tanzania TARURA kutoka Bilioni 700 mpaka Trilioni moja na Milioni mia tisa katika jitihada zake za kuzifungua barabara za lami na za changarawe ili ziweze kupitika kwenye misimu yote.
Dkt. Samia pia ameeleza mipango yake ikiwa atachaguliwa kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 serikali yake itajenga barabara ya mzunguko ya Tabora Mjini itakayokuwa na Kilomita 82 ili kupunguza foleni ya magari Tabora Mjini kwa magari yasiyokuwa na ulazima kupita Katikati ya Mji kuweza kutumia barabara hiyo.
“Tunataka Tabora yenye historia kubwa iwe na hadhi kubwa lakini katika hatua nyingine tunakwenda kujenga madaraja 133 katika barabara tulizoziweka kwenye Ilani, tutaweka taa pia 2300 kwenye barabara kwahiyo Tabora itakwenda kufanya kazi muda wote.” Amesema Dkt. Samia.