Home BUSINESS NIRC: UMWAGILIAJI NGUZO DIRA YA MAENDELEO 2050

NIRC: UMWAGILIAJI NGUZO DIRA YA MAENDELEO 2050

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, amesema kuwa Serikali imefanya uamuzi wa kimkakati kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Mndolwa alieleza hayo wakati wa mjadala maalum wa wadau wa kilimo waliokusanyika kujadili utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2050. Mjadala huo umeandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango (NPC).

“Tangu kupata uhuru, kilimo nchini kimekuwa kikitegemea mvua, jambo linalosababisha kutokuwa na uhakika wa mavuno. Serikali imeona umuhimu wa kuwekeza kwenye umwagiliaji ili kuhakikisha uzalishaji unaendelea kwa uhakika mwaka mzima,” alisema Mndolwa.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa malengo ya Dira 2050, kilimo cha umwagiliaji kinatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hasa katika kufanikisha ndoto ya kufikia uchumi wa kati unaojitegemea.

Mndolwa alibainisha kuwa Tume ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa mabwawa na uchimbaji wa visima, ambapo mitambo ya kisasa ya umwagiliaji itasambazwa kupitia halmashauri ili kuwafikia wakulima walioko maeneo mbalimbali nchini.

“Lengo letu ni kuhakikisha Taifa linaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na wakati huo huo kuboresha maisha ya wananchi kupitia kilimo chenye tija kisichotegemea mvua pekee,” aliongeza.

Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kuwa mshiriki hai katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia na kuwawezesha wakulima kwa elimu na rasilimali za kutosha.