Home BUSINESS WAZIRI NDEJEMBI AITAKA NHC KUELEKEZA KASI UJENZI WA MIRADI YA SAMIA HOUSING...

WAZIRI NDEJEMBI AITAKA NHC KUELEKEZA KASI UJENZI WA MIRADI YA SAMIA HOUSING SCHEME DODOMA 

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dar es Salaam, 28 Julai 2025

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, leo ametembelea makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yaliyopo Kambarage House, jijini Dar es Salaam, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na menejimenti ya Shirika hilo na kupitia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo muhimu ya Serikali.

Katika mazungumzo yake na uongozi wa juu wa NHC, Mhe. Ndejembi alieleza kufurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Shirika hilo katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara nchini. Alisisitiza kuwa NHC ina jukumu kubwa la kuendeleza sekta ya makazi kwa kasi, ubunifu na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa NHC katika maendeleo ya sekta ya makazi. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inaleta tija kwa wananchi na kuakisi thamani ya uwekezaji unaofanyika,” alisema Mhe. Ndejembi.

Katika mkutano huo, Waziri aliwataka viongozi wa NHC kuimarisha usimamizi wa miradi na kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara. Alisema ushirikiano huo ni muhimu ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo na kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.

Akizungumzia miradi inayotekelezwa mkoani Dodoma kupitia Samia Housing Scheme Phase II, Mhe. Ndejembi alielekeza kuharakishwa kwa ujenzi wa nyumba katika maeneo ya Medeli na Njedengwa, huku akiweka mkazo mkubwa kwa timu ya utekelezaji kufuata viwango vya ubora.

“Nawaelekezeni hizi nyumba ambazo mmeanza kujenga misingi yake leo – ziharakisheni huku mkizingatia ubora. Mtawafikia Watanzania wengi zaidi, na kwa hakika, Dodoma itazidi kupendeza,” alisisitiza.

Waziri alifafanua kuwa tayari kuna idadi kubwa ya wateja waliopo jijini Dodoma ambao wana uhitaji mkubwa wa nyumba, na hiyo ni fursa ya Shirika kuwahudumia wananchi kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hammad Abdallah, alimhakikishia Waziri kuwa Shirika linatekeleza kwa makini maelekezo yote yanayotolewa na Wizara. Alimshukuru Mhe. Ndejembi kwa uongozi wake thabiti na msaada wa karibu ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuharakisha utekelezaji wa miradi.

“Tunamshukuru sana Mhe. Waziri kwa uongozi wake bora na maelekezo ya mara kwa mara ambayo yamekuwa mwanga na dira kwetu. Tunajivunia mafanikio tunayoyapata chini ya uongozi wake na tutaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunawafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Bw. Hammad.

Aidha, alieleza kuwa miradi ya Samia Housing Scheme imepokelewa kwa mwitikio mkubwa na wananchi na kwamba NHC imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Ziara ya Mhe. Ndejembi katika Kambarage House ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinafanya kazi kwa weledi, ufanisi na kwa kuzingatia matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa.