Home LOCAL TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA DIRISHA LA UDAHILI SHAHADA YA KWANZA

TCU YATANGAZA KUFUNGULIWA DIRISHA LA UDAHILI SHAHADA YA KWANZA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: Hughes Dugilo,  DSM 

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufunguliwa kwa Awamu ya Kwanza ya udahili wa Shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kuanzia l eo Julai 15, 2025 hadi Ogasti10 mwaka huu, huku ikiainiisha sifa zinazohitajika kwa wanafunzi wanaopaswa kuomba udahili.

Akizungumzia utaratibu wa kutuma maombi ya udahili, Prof. Charles Kihampa amesema maombi yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo muombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda, nakwamba maelekezo mahususi ya jinsi ya kutuma maombi yanatolewa na vyuo husika.

“Udahili na sifa katika programu mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyopatikana katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz)” ameongeza.

Pia ameyataja  masuala muhimu ya kuzingatiwa na waombaji ambayo ni pamoja na kusoma kwa makini na kuelewa mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU, pamoja maelekezo mahususi ya vyuo kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.

Kuingia katika tovuti za vyuo na kuwasiliana na vyuo moja kwa moja ili kujua taratibu 12 kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi.

Akizungumzia waombaji Watanzania wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kuwasilisha vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari Baraza la Taifa au Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa vyeti vya ya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu we sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Pia waombaji ambao siyo Watanzania, wenye vyeti vilivyotolewa ne Mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kutuma maombi ya udahili moja kwa moja kupitia mifumo ya vyuo husika.

Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz), tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza, pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia
vyombo vya habari.

“Tume inatoa wito kwa waombaji wote wa udahili wa Shahada ya Kwanza, endapo watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote linalohusu udahili, wawasiliane moja kwa moja na vyuo husika.

Aidha, iwapo watahitaji maelezo ya jumla wanaweza kuwasiliana na TCU kwa kutumia barua pepe es@tcu.go.tz.

Pia, Tume inawaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.